Mara zote kila mwenye itikadi au akida fulani ana yakini timilifu kuwa akida yake ndio itikadi iliyokuwa sahihi zaidi na ya haki kuliko itikadi nyingine, na kila mmoja anatofautiana na mwenye itikadi nyingine kwa kuthibitisha hilo; pale watu wenye itikadi za kibinadamu zilizoharibika au zilizopotea huthibitisha hilo kwa kudai kuwa wamewakuta baba zao wakifanya hivyo na ya kuwa wao huwafuata wao, Allah Ta’ala amesema, “Na kadhaalika hatukumtuma mwonyaji kwenye mji wowote ila watu wake walio deka kwa starehe walisema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu wanashika dini makhsusi, na sisi tunafuata nyayo zao. Akasema (Mwonyaji): Hata nikikuleteeni yenye uwongofu bora kuliko mlio wakuta nao baba zenu? Wakasema: Sisi tunayakataa tu hayo mliyo tumwa.” (43:23-24)
Na aya nyingine amesema, “Na wanapo ambiwa: Fuateni aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu; wao husema: Bali tutafuata tuliyo wakuta nayo baba zetu. Je, hata ikiwa baba zao walikuwa hawaelewi kitu, wala hawakuongoka? Na mfano wa walio kufuru ni kama mfano wa anaye mpigia kelele asiye sikia ila wito na sauti tu -- ni viziwi, mabubu, vipofu, kwa hivyo hawaelewi. ” (2:170-171)
Na hutoa dalili ya msimamo wao huu kwa kufuata kibubusa bila ya kutumia akili au kufikiria, au kuthibitisha kwa kutumia habari za uongo au zenye makosa, zenye kugongana ambazo hazina dalili juu ya ukweli wake, na bila ya shaka haifai kutolea hoja au dalili kwa dini hizi na mila mbali mbali.
Na kwa sababu haki ni moja sio nyingi, ni muhali itikadi zote hizo kuwa ni sawa, na ni muhali zote hizo kuwa sahihi katika wakati mmoja, la sivyo usawa ungekuwa unapingana, na hili halikubaliki kwa akili iliyosalimika: “…Na lau kuwa imetoka kwa asiye kuwa Mwenyezi Mungu bila ya shaka wangeli kuta ndani yake khitilafu nyingi.” (4:82).
Kama ni hivyo basi dini sahihi ni ipi? Ni vidhibiti gani ambavyo vinaweza kuhukumu kuwa moja ya itikadi hii ni ya kweli na nyingine isiyokuwa hiyo si ya kweli?!
Dini iwe ni kutoka kwa Mungu, yaani kutoka kwa Allah Ta’ala na hiyo iwe imekuja kupitia kwa Malaika miongoni mwa Malaika kwa Mtume ili nae afikishe kwa waja wa Allah; kwa sababu dini ya haki ni dini ya Allah aliyeumba Ulimwengu huu, na Allah Ta’ala ndiye ambaye analipa na kuwahesabu viumbe Siku ya Kiama kwa dini ambayo amewateremshia, Allah amesema: “Hakika Sisi tumekuletea wahyi wewe kama tulivyo wapelekea wahyi Nuhu na Manabii walio kuwa baada yake. Na tulimpelekea wahyi Ibrahim na Ismail na Is-haka na Yaakub na wajukuu zake, na Isa na Ayub na Yunus na Harun na Suleiman, na Daud tukampa Zaburi. Na Mitume tulio kwisha kukuhadithia kabla yake, na Mitume wengine hatukukuhadithia. Na Mwenyezi Mungu alinena na Musa kwa maneno. Mitume hao ni wabashiri na waonyaji, ili watu wasiwe na hoja juu ya Mwenyezi Mungu baada ya kuletewa Mitume. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.” (4:163-165).
Na kulingana na jambo hilo ni kuwa dini yoyote ambayo mtu anajinasibisha nayo na sio kwa Allah ni dini batili bila ya shaka, na dini ambayo ataiendeleza mwanadamu na kuiongezea ni batili vile vile bila ya chembe ya shaka, wala mwenye kuiendeleza au kuibadilisha ni mwenye kujua yale yanayowafaa watu kuliko Allah muumba: “Asijue aliye umba, naye ndiye Mjua siri, Mwenye khabari?” (67:14)
Vinginevyo mwenye kuendeleza au kuweka sheria ni Allah Muumba mwenye kujua kinachowafaa viumbe vyake, ametakasika Allah kwa hilo: “Je, wanataka dini isiyo kuwa ya Mwenyezi Mungu, na hali kila kilichomo mbinguni na katika ardhi kimesilimu kwa kumt’ii Yeye kikipenda kisipende, na kwake Yeye watarejeshwa?” (3:83)
Na Allah akasema tena, “La! Naapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye muamuzi katika yale wanayo khitalifiana…” (4:65).
Dini hiyo iwalinganie watu kumuabudu Allah Ta’ala na kuharamisha ushirikina; hivyo basi Da’wah katika tawhidi ndio msingi wa da’wah ya Mitume yote, na ushirikina na upagani ndio ambayo inakwenda kinyume kabisa na maumbile sahihi ya mwanadamu na akili zilizoongoka, Allah Ta’ala amesema: “Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimfunulia ya kwamba hapana mungu isipo kuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu” (21:25)
Na kila Mtume alisema maneno yafuatayo kwa watu wake: “…Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya Siku iliyo kuu.” (7:59),
Na kwa hilo basi dini yoyote ambayo itakiri ushirikina, au kumshirikisha Nabii au Malaika au walii au mtu au jiwe pamoja na Allah, basi dini hiyo ni batili, kwani ibada ni kwa Allah pekee hana mshirika pamoja nae, na upagani na ushirikina ni upotevu ulio dhahiri, na kila dini hata kama ikiwa kutoka kwa Allah na ikaingizwa ndani yake ushirikina basi dini hiyo vile vile ni batili, Allah Ta’ala ametupigia mfano; aliposema, “Enyi watu! Unapigwa mfano, basi usikilizeni. Hakika wale mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu, hawatoumba hata nzi ijapo kuwa watajumuika kwa hilo. Na nzi akiwapokonya kitu hawawezi kukipata kwake. Amedhoofika kweli huyo mwenye kutaka na mwenye kutakiwa. Hawakumuadhimisha Mwenyezi Mungu anavyo stahiki kuadhimishwa. Hakika Mwenyezi Mungu bila ya shaka ni Mwenye kushinda.” (22:73-74).
Dini hiyo iafikiane na maumbile sahihi, Allah amesema: “Basi uelekeze uso wako sawasawa kwenye Dini - ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilo waumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo Dini iliyo nyooka sawa. Lakini watu wengi hawajui.” (30:30),
Na maumbile sahihi ni kila ambacho Allah amempa mwanadamu na ikawa kwake ni sehemu ya maumbile yake, kwani haiwezi kuwa dini ambayo haifai maumbile ya mwanadamu, vinginevyo basi Muumba asingekuwa na uwezo wa kuweka sheria ya dini, na jambo hii ni muhali na la kishirikina.
Dini hiyo iafikiane na akili sahihi; kwa sababu dini sahihi ni sheria ya Allah na akili sahihi ni maumbile aliyoyaumba Allah, na ni muhali sheria ya Allah na maumbile yake kugongana, Allah amesema: “Je! Hawatembei katika ardhi ili wapate kuwa na nyoyo zao za kuzingatia, au masikio ya kusikilia? Kwani hakika si macho yanayo pofuka, lakini zinazo pofuka ni nyoyo ziliomo vifuani.” (22:46)
Na Akasema, “Hakika katika mbingu na ardhi ziko Ishara kwa Waumini. Na katika umbo lenu na katika wanyama alio watawanya zimo Ishara kwa watu wenye yakini. Na kupishana usiku na mchana, na riziki anayo iteremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, na kwayo akaifufua ardhi baada ya kufa kwake, na mabadiliko ya upepo, ni Ishara kwa watu wenye akili. Hizi Aya za Mwenyezi Mungu tunakusomea kwa haki; basi hadithi gani watakayo iamini baada ya Mwenyezi Mungu na Aya zake? ” (45:3-6)
Hivyo basi haiswihi kuwa dini ya kweli imejaa upotevu na migongano kiasi tunapata baadhi yake ni tofauti kabisa na nyingine, na huu ni mgongano wa akili sahihi, hivyo basi haiwezi kuamrisha kisha ikaja amri nyingine inayogongana nayo, wala isiharamishe jambo au kuiruhusu kwa kundi maalumu kisha kulihamisha kwa kundi jingine, au kutofautisha baina ya vyenye kufanana au kuvikusanya baina ya vyenye kugongana,
Allah Ta’ala amesema, “Hebu hawaizingatii hii Qur’ani? Na lau kuwa imetoka kwa asiye kuwa Mwenyezi Mungu bila ya shaka wangeli kuta ndani yake khitilafu nyingi.” (4:82)
Bali ni lazima iwe imejengwa kwa dalili nyingi mbali mbali zilizo wazi, Allah amesema: “…Leteni ushahidi wenu kama nyinyi ni wasema kweli.” (2:111)