Mwanadamu kwa hali yoyote hawezi kuishi bila Dini, na kwa sababu mwanadamu ni mtu mwenye tabia ya kuingiliana na watu na hawezi kuishi peke yake huku akijitenga na jamii, nae vile vile katika maumbile yake ni mtu mwenye dini hawezi kuishi maisha ya sawa sawa bila kuwa na dini, swala la mtu kuwa na dini ni suala la kimaumbile na tabia ya asili ya mwanadamu na hakuna dalili kubwa yenye kuthibitisha hilo kuliko ile hali ya mwanadamu kumtegemea Mwenyezi Mungu katika hali ya shida na dharura, Allah Ta’ala amesema, “Na wanapo panda katika marikebu, humwomba Mwenyezi Mungu kwa kumsafia ut’iifu. Lakini anapo wavua wakafika nchi kavu, mara wanamshirikisha.” (29:65)
Kama ambavyo mtu aliyetengeneza mashine ndiye mwenye kufahamu zaidi mahitajio yake vivyo hivyo na muumbaji huwajua zaidi viumbe wake na mahitaji yao, “Asijue aliye umba, naye ndiye Mjua siri, Mwenye khabari? ”(67:14)
Na kwa sababu Muumba ni Mrehemu na Ghafuri Mkarimu; amewawekea watu sharia ya Dini ili Nafsi zao zihuishwe na maisha yao yadhibitiwe, Allah Ta’ala amesema, “Enyi mlio amini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapo kuitieni jambo la kukupeni uzima wa milele….” (8:24),
Na kwa hilo basi hata yule ambaye anakwenda kinyume na maumbile sahihi na anadai kumkana Allah Ta’ala, wao ni ndani ya Nafsi zao wanajua uongo wa kukana kwao, Allah amesema, “Na wakazikataa kwa dhulma na kujivuna, na hali ya kuwa nafsi zao zina yakini nazo. Basi angalia ulikuwaje mwisho wa mafisadi!” (27:14)
Na huenda hilo likaonekana kwa uwazi zaidi wakati wa zahama na matatizo zaidi, Allah amesema, “Sema: Mwaonaje ikikujieni adhabu ya Mwenyezi Mungu, au ikakufikieni hiyo Saa - mtamwomba asiye kuwa Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi ni wakweli? Bali Yeye ndiye mtakaye mwomba, naye atakuondoleeni mnacho mwombea akipenda. Na mtasahau hao mnao wafanya washirika wake.” (6:41-42)
Kadhalika katika Surat Zumar amesema: “Na taabu inapo mfikia mtu humwomba Mola wake Mlezi naye ameelekea kwake. Kisha akimpa neema kutoka kwake, husahau yale aliyo kuwa akimwitia zamani, na akamfanyia Mwenyezi Mungu washirika ili apoteze watu njia yake. Sema: Starehe na ukafiri wako kwa muda mchache. Kwani hakika wewe utakuwa miongoni mwa watu wa Motoni. ” (39:8).
Wanadamu wote wapo katika maumbile ya asili waliyoumbwa nayo na Allah Ta’ala katika kumuabudu yeye kwa mkono wake kheri na shari kufanya ayatakayo na kuhukumu atakavyo, Allah Ta’ala amesema: “Na ikiwa Mwenyezi Mungu akikugusisha madhara, basi hapana wa kukuondolea hayo ila Yeye. Na ikiwa akikugusisha kheri, basi Yeye ndiye Mwenye uweza wa kila kitu.” (6:17)
Na katika Surat Faatwir amesema: “Rehema ambayo Mwenyezi Mungu anawafungulia watu hapana wa kuizuia. Na anayo izuia hapana wa kuipeleka isipo kuwa Yeye. Naye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.” (35:2).
Mwanadamu ana nguvu za aina mbili: Nguvu ya elimu na nguvu ya matakwa yake, na kwa kadiri ya juhudi yake katika kutekeleza nguvu hizo mbili mwanadamu huyo hufikia malango yake aliyojipangia na vivyo hivyo ndivyo mwanadamu apatavyo furaha.
Ama nguvu ya kwanza (nguvu ya elimu) kwa kadiri ya maarifa yake kwa Allah, kwa majina yake na sifa zake, na yanayopasa kwake katika maamrisho na makatazo, kitabia na kimaadili na vipi ilivyo njia ya ukuruba na kuwa juu ya daraja za mwenye kufuata, na yote yenye kupelekea katika elimu ya ndani kuhusu Nafsi za wanadamu na maradhi yake na jinsi ya kuyashinda hayo, na kwa maadui zake na kila chenye kuzuia baina yake na Mola wake, mbali na mtu kukwea daraja za juu za kutakasa tabia yake iwe ya kiungu kiasi cha kupanda juu kufikia roho za juu na hima za juu, mbali kabisa na mambo ya hovyo kwa lengo la kupata maslahi ya kidunia na matamanio yake, kwa kiasi hicho ndio kimada unapokuwa daraja ya uja wa mtu kwa Allah Ta’ala na nafasi yake, bali na furaha yake duniani sembuse ya akhera.
Nguvu hii ya kielimu ndio masurufu na msaada wa nguvu ya matakwa ya mtu, ambayo yatamuongoza katika uongofu pamoja na kuthibiti na kufanya mambo mazuri, Allah Ta’ala amesema: “Enyi mlio amini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapo kuitieni jambo la kukupeni uzima wa milele….”” (8:24)
Na haya madhehebu ya wakanayo Mungu na Dini yanatangaza kufilisika kwao kwa kutekeleza kwao raha za kiwiliwili sembuse kushibisha mahitajio ya kiroho, madhehebu haya yameshindwa kabisa kumhakishia mwanadamu furaha ya kweli vyovyote watakavyopeana kauli nzuri na kupamba kauli zao kwa ghururi.
Mwanadamu anamuelekea nani katika matatizo yake na misiba yake! Anategemea nguzo imara, anaelekea kwa Allah Ta’ala; penye nguvu, matarajio, subira na kutegemea kwema na kumwachia mambo yote yeye. Allah amesema; “Wale walio amini na zikatua nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Hakika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndio nyoyo hutua! ” (13:28).
Hadi hapo atakapoonja uchungu wa moto kwa dhulma ndipo atakapokuwa na yakini kuwa ulimwengu huu una Mola, na ambaye anamnusuru aliyedhulumiwa hata kama, ni baada ya muda kupita, na ya kuwa kuna siku ya mwisho ambayo kila mmoja atalipwa alichokichuma, na mtu mwema kulipwa mema yake na muovu kulipwa maovu yake na hivyo basi kifua chake kuwa imara kwa tumaini na yakini kwa Allah. Allah Ta’ala amesema: “Je! Aliye yafuata ya kumridhisha Mwenyezi Mungi ni kama yule aliye stahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, na makaazi yake yakawa Jahannamu? Napo ni mahala pabaya pa kurejea. ” (3:162).
Kinyume na yaliyotangulia; yule ambaye amepoteza maarifa yake kwa Allah Ta’ala na kumuamini basi mtu huyo amepoteza nguvu zake zote, na kadhalika atakuwa amepoteza raha, tumaini na furaha, na atakuwa anaishi baina ya hamu na huzuni, hana utulivu ndani ya nafsi yake, hamu yake kubwa ni kutekeleza na kufanikisha matamanio yake hajui malengo ya maisha yake, wala maana ya kuwepo kwake hapa ulimwenguni. Bali mtu huyu anaishi akibabaika hajui afanye nini, akitafuta furaha, akifuata matamanio yake, lakini anarudi nyuma kiasi cha kuwa ni mnyama au aliyepotea zaidi, Allah Ta’ala amesema: “Au wewe unadhani kwamba wengi wao wanasikia au wanaelewa? Hao hawakuwa ila ni kama nyama hoa tu, bali wao wamepotea zaidi njia.”(25:44),
Na ikitokea mtu huyu kapatwa na msiba basi kuangukia kuwa ni muhanga wa angamizo la nafsi na angaiko na babaiko lake la ndani, “Na atakaye jiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa kipofu.”. (20:124)
Ni tofauti kubwa sana baina ya mtu mwenye kumjua Mola wake, na kujua ukubwa wake na akajua kinachompasa kwake kwa Mola wake na kuijali kwake kumridhisha Mola wake, akifuata sheria zake, akitii maamrisho yake na kuacha makatazo yake, Na akajua kuwa ni mwenye haja ya kudumu kwa Mola wake katika madogo na makubwa, katika mambo dhalili na matukufu, na katika kila wakati Allah Ta’ala amesema: “Enyi watu! Nyinyi ndio wenye haja kwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujitosha, Msifiwa.”(35:15).
Na mtu mwingine dhana na mawazo yamemtupa katika taabu na kiza na shida, akipapasa kwa kupepesuka kama vile kipofu hapa na pale, moyo wake ukiwa umejaa shaka na wasiwasi, kila akijaribu kukamata au kushika furaha anajikuta yupo katika mazigazi baada ya mazigazi, na hata akipata ladha za dunia na matamanio yake, na hata akipanda cheo na daraja za juu, Je, mtu atakayemkosa Allah atapata nini? Na atakayempata Allah atakuwa amekosa nini?