Tarekh ya mitume:utangulizi mkuu

Tarekh ya mitume:utangulizi mkuu

Tarekh ya mitume:utangulizi mkuu

Imani kwa mitume

Watu walikuwa katika uongofu na wakatofautiana, Allah akatuma Mitume, ili awafundishe watu na awaonye:“Yeye ndiye aliye mpeleka Mtume kwenye watu wasio jua kusoma, awasomee Aya zake na awatakase, na awafunze Kitabu na hikima, ijapo kuwa kabla ya haya walikuwa katika upotofu ulio dhaahiri” (62:2)

Lakini watu wakagawanyika kulingana na da’wah ya Mitume katika makundi mawili; kundi lililokubali (lililosadikisha) Mitume na kuamini, na kundi lililokadhibisha Mitume na kuwakana na kile walichokuja nacho, waliwakadhibisha kwa ujeuri; “Watu wote wa likuwa ni umma mmoja. Mwenyezi Mungu akapeleka Manabii wabashiri na waonyaji. Na pamoja nao akateremsha Kitabu kwa Haki, ili kihukumu baina ya watu katika yale walio khitalifiana. Na wala hawakukhitalifiana ila wale walio pewa Kitabu hicho baada ya kuwafikia hoja zilizo wazi, kwa sababu ya uhasidi baina yao. Ndipo Mwenyezi Mungu kwa idhini yake akawaongoa walio amini kwendea haki katika mambo waliyo khitalifiana. Na Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye kwenye Njia Iliyo Nyooka.” (2:213)

Na walikadhibisha kwa kiburi na kufuata matamanio yao, “…Basi kila walipo kufikieni Mitume kwa yale ambayo hayapendwi na nafsi zenu, mlijivuna; wengine mkawakanusha, na wengine mkawauwa.” (2:87).

Allah Ta’ala ameamrisha Mitume wote waaminiwe, “Semeni nyinyi: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na yale tuliyo teremshiwa sisi, na yaliyo teremshwa kwa Ibrahim na Ismail na Is-hak na Yaakub na wajukuu zake, na waliyo pewa Musa na Isa, na pia waliyo pewa Manabii wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi; hatutafautishi baina ya yeyote katika hao, na sisi tumesilimu kwake.” (2:136),

Na akawaahidi watakaoamini Mitume kupata furaha, na uokozi hapa duniani na akhera, na akawakamia watakaokufuru na kuupa mgongo kupata khasara na tabu hapa duniani kabla ya kesho akhera, Allah amesema,“Na atakaye fanya urafiki na Mwenyezi Mungu na Mtume wake na walio amini, basi hakika kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kushinda.” (5:56)

Na akasema vile vile:“Wale walio amini na zikatua nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Hakika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndio nyoyo hutua! Wale walio amini na wakatenda mema watakuwa na raha na marejeo mazuri.” (13:28-29)

Na akasema kwa wale waliokufuru Mitume:“Msiwadhanie walio kufuru kwamba watashinda katika nchi. Na makaazi yao ni Motoni, na hakika ni maovu kweli marejeo yao” (24:57).

Maadui wa mitume

Kila Mtume alikuwa na adui zake, Allah amesema:“Na kadhaalika tumemfanyia kila Nabii maadui mashet’ani wa kiwatu, na kijini, wakifundishana wao kwa wao maneno ya kupamba-pamba, kwa udanganyifu. Na angeli penda Mola wako Mlezi wasingeli fanya hayo. Basi waache na wanayo yazua.” (6:112),

Kisha waliokadhibisha waliwafanyia jeuri Mitume na kuwafanyia uadui, na wakawafanyia istihzai na kuwadharau, Allah amesema:“Na hakuwafikia Mtume ila walimkejeli.” (15:11)

Na akasema Mtukuka:“Na hawajii Nabii yeyote ila walikuwa wakimkejeli.” (43:7)

Na akasema Mtukuka: “Na hakika Mitume walio kabla yako walifanyiwa kejeli, lakini walio wafanyia kejeli wakaja kuzungukwa na yale yale waliyo kuwa wao wanayafanyia kejeli.” (6:10)

Na hali kadhalika wakawatishia kuwafukuza na kuwatoa katika miji yao, au warudi katika dini zao, Allah amesema, “Na walio kufuru wakawaambia Mitume wao: Tutakutoeni katika nchi yetu, au mrudi katika mila yetu. Basi Mola wao Mlezi aliwaletea wahyi: Hakika tutawaangamiza walio dhulumu!” (14:13),

Vitisho hivyo vikafikia kiasi cha kuwauwa, “…Na kila taifa lilikuwa na hamu juu ya Mtume wao wamkamate….” (40:5),

Yaani kumuuwa, kiasi cha miongoni mwao kuuwa Mitume wao, “…Basi kila walipo kufikieni Mitume kwa yale ambayo hayapendwi na nafsi zenu, mlijivuna; wengine mkawakanusha, na wengine mkawauwa” (2:87),

Mwenyezi Mungu baada ya hapo akawaangamiza waliokadhibisha na akadhihirisha dini ya Mitume, kama alivyosema Allah Ta’ala: “Mwenyezi Mungu ameandika: Hapana shaka Mimi na Mtume wangu tutashinda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kushinda.” (58:21)

$Marcel.jpg*

Marcel Boisard

Mwanafikra wa Kifaransa
Kutoka katika taa moja.
“Hakukuwepo ndani ya ujumbe wa Muhammad kubatilisha yaliyoteremshwa kabla yake; bali ni kusadikisha upungufu uliovikumba vitabu vya mbinguni kama vile; kubadilisha na kuvunja sheria, na ukalazimishwa kusafisha mafundisho ya Mitume waliyotangulia katika kila kosa. Hivyo kupanuka ndani yake na kuenea kwake: ili iwafae wanadamu wote katika kila zama na mahali.”

Na akasema Mtukuka: “Na bila ya shaka neno letu lilikwisha tangulia kwa waja wetu walio tumwa. Ya kuwa wao bila ya shaka ndio watakao nusuriwa. ” (37:171-172)

Na Allah aliokoa Mitume wake wote, kama Allah alivyosema: “Na tukawaokoa wale walio amini na walio kuwa wanamchamngu.” (27:53)

Na akasema vile vile: “Na tukawaokoa walio amini na wakawa wanamcha-mngu.” (41:18)

Na kila Mtume aliyekwenda kwa watu wake na kulazimiana na yanayonasibiana nao kutengeneza maisha yao na kuwatakasa; Basi ambaye atakadhibisha Mtume mmoja, ni kama vile amewakadhibisha Mitume wote, yule ambae hamuamini Issa (‘Alahyi Salaam) basi kihakika hatokuwa amemwamini Musa (‘Alahyi Salaam), na Muhammad akafuta ujumbe wa Issa (‘Alahyi Salaam) Allah amesema: “Na tumekuteremshia wewe, kwa haki, Kitabu hichi kinacho sadikisha yaliyo kuwa kabla yake katika Vitabu na kuyalinda. Basi hukumu baina yao kwa aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao ukaacha Haki iliyo kujia….” (5:48)

Kwa hivyo basi ambaye hatomuamini Muhammad kihakika hatakuwa amemuamini Issa (‘Alahyi Salaam). Na kuwa ni lazima kuwe Mtume wa mwisho kwa ajili ya watu wote na mahali pote, na sio kwa muda maalumu au fulani, vinginevyo Walimwengu wangepotea na kuangamia bila ya kuwepo msaada wa Wahyi kutoka kwa Muumba wa Ardhi na Mbingu. Hivyo basi Muhammad akawa ndiye Mtume wa mwisho Allah amesema, “Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Manabii, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu” (33:40)

Maumbile ya mwanadamu

$Bashir_Shaad.jpg*

Bashir Shaad

Mhubiri wa India.
Hatutofautishi baina yao.
“Qur-aan tukufu ni kitabu cha pekee ambacho kinakiri uwepo wa vitabu vingine kutoka mbinguni. Wakati ambapo tunaona vitabu vyote hivyo kila kimoja kinakataa vingine.”

Tunaanzia pale Allah alipotaka kumuumba mwanadamu mpaka kumtoa Adam Peponi na kuteremka ardhini, “Na pale Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Mimi nitamweka katika ardhi Khalifa (mfwatizi), wakasema: Utaweka humo atakaye fanya uharibifu humo na kumwaga damu, hali sisi tunakutakasa kwa sifa zako na tunakutaja kwa utakatifu wako? Akasema: Hakika Mimi nayajua msiyo yajua. Na akamfundisha Adam majina ya vitu vyote, kisha akaviweka mbele ya Malaika, na akasema: Niambieni majina ya hivi ikiwa mnasema kweli. *Wakasema: Subhanaka, Wewe umetakasika! Hatuna ujuzi isipokuwa kwa uliyo tufunza Wewe. Hakika Wewe ndiye Mjuzi Mwenye hikima. Akasema: Ewe Adam! Waambie majina yake. Basi alipo waambia majina yake alisema: Sikukwambieni kwamba Mimi ninajua siri za mbinguni na za duniani, na ninayajua mnayo yadhihirisha na mliyo kuwa mnayaficha? Na tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam, wakamsujudia wote isipo kuwa Iblis, alikataa na akajivuna na akawa katika makafiri. Na tulisema: Ewe Adam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani, na kuleni humo maridhawa popote mpendapo, lakini msiukaribie mti huu tu; mkawa katika wale walio dhulumu. Lakini Shet’ani aliwatelezesha hao wawili na akawatoa katika waliyo kuwamo, na tukasema: Shukeni, nanyi ni maadui nyinyi kwa nyinyi. Katika ardhi yatakuwa makaazi yenu na starehe kwa muda. Kisha Adam akapokea maneno kwa Mola wake Mlezi, na Mola wake Mlezi alimkubalia toba yake; hakika Yeye ndiye Mwingi wa kukubali toba na Mwenye kurehemu. Tukasema: Shukeni nyote; na kama ukikufikieni uwongofu utokao kwangu, basi watakao fuata uwongofu wangu huo haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika. Na wenye kukufuru na kuzikanusha ishara zetu, hao ndio watakao kuwa watu wa Motoni, humo watadumu. ” (2:30-39).

Kisha baada ya hapo watu wakaupa mgongo uongofu na haki, ndipo alipotuma Mitume wake, Mitume wakafuatana pamoja na sheria zao; “Amekuamrisheni Dini ile ile aliyo muusia Nuhu na tuliyo kufunulia wewe, na tuliyo wausia Ibrahim na Musa na Isa, kwamba shikeni Dini wala msifarikiane kwayo.” (42:13)

Kisha wakafuatana Mitume wa Allah kutokea Idriss hadi Nuhu, Ibrahim, Ismail, Musa, Issa na Muhammad (Swalawatu Llahi Wasalamuhu alayhim jami’an). Allah ametutajia visa vyao na kutujulisha habari zao, hapa tutataja kidogo kuhusu visa vya baadhi yao; kwani visa vyao vimejaa mazingatio kwa wenye akili, Allah Ta’ala amesema: “Kwa hakika katika hadithi zao limo zingatio kwa wenye akili. Si maneno yaliyo zuliwa, bali ni ya kusadikisha yaliyo kabla yake, na ufafanuzi wa kila kitu, na ni uwongofu na rehema kwa kaumu yenye kuamini” (12:111);