Ibrahim (‘Alahyi Salaam) Mtume wa Tawhidi, hilo linadhihiri katika Historia yake; hivyo ndio maana Allah akamsifu kwa kusema: “Hakika Ibrahim alikuwa mfano mwema, mnyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu, mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.” (16:120);
Ibrahim aliishi pamoja na kaumu ya washirikina, bali baba yake alikuwa mmoja wa wanaoabudu masanamu na mmoja miongoni mwa wanaoyatengeneza na kuyaabudu, Ibrahim akaanza kujadiliana na baba yake pamoja na kaumu yake: “Na pale Ibrahim alipo mwambia baba yake, Azar: Unayafanya masanamu kuwa ni miungu? Hakika mimi nakuona wewe na watu wako mmo katika opotofu ulio wazi.” (6:74)
Na akapinga yaliyokuwa kwa kaumu yake kwa hoja madhubuti ushirikina wao na akawa anaangalia katika alama na dalili za kuwepo kwake Allah Ta’ala: “Na ulipo muingilia usiku akiona nyota, akasema: Huyu ni Mola Mlezi wangu. Ilipo tua akasema: Siwapendi wanao tua.” (6:76);
Yaani: kuzama kwa nyota: “akasema: Siwapendi wanao tua. Alipo uona mwezi unachomoza…” (6:76-77),
Yaani: Kuchomoza kutoka kwenye upeo wa macho, na akaona baadhi ya watu wakiyaabudu: “…alisema: Huyu ndiye Mola Mlezi wangu…” (6:77).
Akapinga matendo yao, huku akistaajabia ibada zao!! Aliitumia fursa hiyo: “…Ulipotua…” (6:77);
Yaani kupotea chini ya upeo wa macho, alielekea kwa watu wake na kuwaambia: “…akasema: Kama Mola Mlezi wangu hakuniongoa, nitakuwa katika kaumu walio potea. …Na alipo liona jua linachomoza” (6:77-78),
Na akawaona watu wakinyenyekea mbele yake: “…akasema: Huyu ndiye Mola Mlezi wangu. Huyu mkubwa kuliko wote….” (6:78)
Akapinga matendo yao!! Akashangazwa ni kwa nini wamefanya jua kuwa Mungu wao?! “…Lilipo tua…” (6:78),
Na kupotea machoni, aliwaelekea watu wale ambao walikuwa wakiiabudia, akawaambia: “…alisema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika hayo mnayo fanyia ushirikina. …Hakika mimi nimeuelekeza uso wangu sawa sawa kwa aliye ziumba mbingu na ardhi, wala mimi si miongoni mwa washirikina.” (6:78-79).
Na alikuwa akimpa sana mawaidha baba yake na kumkataza ushirikina kwa utulivu, adabu na mantiki: “Sema: Nani anaye kulindeni usiku na mchana na Arrahmani Mwingi wa Rehema? Bali wao wanapuuza kumkumbuka Mola wao Mlezi. Au wao wanao miungu watao weza kuwakinga nasi? Hao hawawezi kujinusuru nafsi zao, wala hawatalindwa nasi! Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka umri ukawa mrefu kwao. Je, hawaoni ya kwamba Sisi tunaifikia ardhi tukiipunguza ncha zake? Basi je! Hao ni wenye kushinda? Sema: Mimi nakuonyeni kwa Wahyi. Na viziwi hawasikii wito wanapo onywa.” (21:42-45).
Kwa bahati mbaya jibu la baba yake lilikuwa kali: “(Baba) akasema: Unaichukia miungu yangu, ewe Ibrahim? Kama huachi, basi lazima nitakupiga mawe. Na niondokelee mbali kwa muda!” (19:46).
Jibu la Ibrahim lilikuwa la adabu ya hali ya juu, huruma na upole: “(Ibrahim) akasema: Salamun a’laika! Amani iwe juu yako! Mimi nitakuombea msamaha kwa Mola wangu Mlezi. Hakika Yeye ananihurumia sana. Nami najitenga nanyi na hayo mnayo yaabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Na ninamwomba Mola wangu Mlezi; asaa nisiwe mwenye kukosa bahati kwa kumwomba Mola wangu Mlezi.” (19:47-48)
Ibrahim aliendelea kuwalingania watu wake na baba yake kwa Allah na tawhidi yake na kuacha ushirikina, lakini watu wake hawakumuitikia Ibrahim na wakaendeea na ushirikina: “Na watu wake wakamhoji. Akasema: Je, mnanihoji juu ya Mwenyezi Mungu, na hali Yeye ameniongoa? Wala siogopi hao mnao washirikisha naye, ila Mola wangu Mlezi akipenda kitu. Mola wangu Mlezi amekusanya ilimu ya kila kitu. Basi je, hamkumbuki? Na vipi nivikhofu hivyo mnavyo vishirikisha, hali nyinyi hamkhofu kuwa nyinyi mmemshirikisha Mwenyezi Mungu…” (6:80-81),
Na kwa mara nyingine akawaambia: “Alipo mwambia baba yake na kaumu yake: Mnaabudu nini?” (26:70)
Wakamjibu: “Wakasema: Tunaabudu masanamu, daima tunayanyenyekea” (26:71), “Akasema: Je! Yanakusikieni mnapo yaita? Au yanakufaeni, au yanakudhuruni?” (26:72-73),
Likawa jibu la kipumbavu ambalo halitumii akili wala mantiki, kwa kuiga tu: “Wakasema: Bali tumewakuta baba zetu wakifanya hivyo hivyo.” (26:74)
Akawajibu kwa kutumia tawhidi halisi kwa hoja na akili na busara: “Je! Mmewaona hawa mnao waabudu- Nyinyi na baba zenu wa zamani? Kwani hakika hao ni adui zangu, isipo kuwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. Ambaye ndiye aliye niumba, na Yeye ndiye ananiongoa, Na ambaye ndiye ananilisha na kuninywesha. Na ninapo ugua ni Yeye ndiye anaye niponesha. Na ambaye atanifisha, na kisha atanihuisha. Na ambaye ndiye ninaye mtumai kunisamehe makosa yangu Siku ya Malipo. Mola wangu Mlezi! Nitunukie hukumu na uniunganishe na watendao mema. Na unijaalie nitajwe kwa wema na watu watakao kuja baadaye. Na unijaalie katika warithi wa Bustani za neema. Na umsamehe baba yangu, kwani hakika alikuwa miongoni mwa wapotovu.” (26:75-86).
Ilipofika sikukuu ya kaumu ile, mfalme pamoja na watu wake walikwenda uwanjani jangwani; ili watekeleze na kusherehekea sikukuu huko, Ibrahim hakutoka pamoja nao; walipondoka: “Nao wakamwacha, wakampa kisogo. Basi akaiendea miungu yao kwa siri, akaiambia: Mbona hamli? Mna nini hata hamsemi? Kisha akaigeukia kuipiga kwa mkono wa kulia. ” (37:90-93),
Waliporudi wakakuta miungu yao imevunjwa, watakuwaje ni Miungu ambayo haiwezi kujitetea! Walikuja upesi: “Wakasema: Nani aliye ifanyia haya miungu yetu? Hakika huyu ni katika walio dhulumu. Wakasema: Tumemsikia kijana mmoja akiwataja. Anaitwa Ibrahim. Wakasema: Mleteni mbele ya macho ya watu, wapate kumshuhudia! Wakasema: Je! Wewe umeifanyia haya miungu yetu, ewe Ibrahim? ” (21:59-62),
Akawajibu kwa hoja kubwa: “Akasema: Bali amefanya hayo huyu mkubwa wao. Basi waulizeni ikiwa wanaweza kutamka.” (21:63)
Wakawa wadogo mbele ya hoja ile: “Basi wakajirudi nafsi zao, wakasema: Hakika nyinyi mlikuwa madhaalimu! Kisha wakarejea kwenye ule ule upotovu wao wakasema: Wewe unajua kwamba hawa hawesemi.” (21:64-65)
Akawajibu kwa hoja kubwa yenye nguvu: “Akasema: Basi nyinyi mnawaabudu asiye kuwa Mwenyezi Mungu wasio kufaini kitu wala kukudhuruni? Aibu yenu nyinyi na hivyo mnavyo viabudu badala ya Mwenyezi Mungu! Basi nyinyi hamtii akilini?” (21:66-67)
Wakataka kulipa kisasi baada ya kukosa hoja, mantiki na dalili: “Wakasema: Mchomeni moto, na muinusuru miungu yenu, ikiwa nyinyi ni watendao jambo!” (21:68)
Allah akamuokoa: “Sisi tukasema: Ewe moto! Kuwa baridi na salama kwa Ibrahim! Wao walimkusudia maovu, lakini Sisi tukawafanya wao ndio walio khasiri.” (21:69-70).
Baada ya Allah kumuokoa, akarudi na kujadiliana na mfalme wao: “Hukumwona yule aliye hojiana na Ibrahim juu ya Mola wake Mlezi kwa sababu Mwenyezi Mungu alimpa ufalme? Ibrahim alipo sema: Mola wangu ni yule ambaye huhuisha na kufisha….” (2:258),
Mbele ya hoja hii yenye nguvu iliyo wazi imekuja kuwa jibu la (mfalme) mpumbavu: “…Yeye akasema: Mimi pia nahuisha na kufisha…” (2:258),
Ibrahim hakubishana nae kwenye kuropoka huku, na kutoka katika mjadala huu kuwa anaweza kumuua mtu na kumuacha mtu: “…Ibrahim akasema: Mwenyezi Mungu hulichomozesha jua mashariki, basi wewe lichomozeshe magharibi. Akafedheheka yule aliye kufuru; na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu.” (2:258)
Udhaifu wa hoja, dalili na mantiki yao ukadhihirika; na baada ya mjadala Ibrahim akataka aone waziwazi namna ambayo Mola wake atahuisha: “Na alipo sema Ibrahim: Mola wangu Mlezi! Nionyeshe vipi unavyo fufua wafu. Mwenyezi Mungu akasema: Kwani huamini? Akasema: Hasha! Lakini ili moyo wangu utue. Akamwambia: Twaa ndege wane na uwazoeshe kwako, kisha uweke juu ya kila kilima sehemu, kisha wete, watakujia mbio. Na ujue kwamba hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu, na Mwenye hikima.” (2:260).
Allah akamuamrisha Ibrahim pamoja na mwanae Ismail kusafisha nyumba ya Allah ya Makka kutokana na ushirikina na masanamu: “…Na tuliagana na Ibrahim na Ismail: Itakaseni Nyumba yangu kwa ajili ya wanao izunguka kwa kut’ufu na wanao jitenga huko kwa ibada, na wanao inama na kusujudu. Na alipo sema Ibrahim: Ee Mola wangu Mlezi! Ufanye huu uwe mji wa amani, na uwaruzuku watu wake matunda, wale wanao muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Akasema: Na mwenye kukufuru pia nitamstarehesha kidogo, kisha nitamsukumiza kwenye adhabu ya Moto, napo ni pahala pabaya mno pa kurejea. Na kumbukeni Ibrahim na Ismail walipo inyanyua misingi ya ile Nyumba wakaomba: Ewe Mola Mlezi wetu! Tutakabalie! Hakika Wewe ndiye Msikizi Mjuzi. Ewe Mola Mlezi wetu! Tujaalie tuwe ni wenye kusilimu kwako, na pia miongoni mwa vizazi vyetu wawe umma ulio silimu kwako. Na utuonyeshe njia za ibada yetu na utusamehe. Bila shaka Wewe ndiye Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.” (2:125-128).