Mitume na Manabii ambao Allah amewatuma kwa waja wake ni lazima Allah awasimamishie hoja na dalili zinazobainisha ukweli wa Da’wah yao, yenye kuhakikisha kuwa wao ni Mitume wa Allah ili hoja isimame kwa watu, na kusiwe na udhuru kwa kutowasadikisha na kuwatii, Allah amesema: “Kwa hakika tuliwatuma Mitume wetu kwa dalili waziwazi” (57:25).
Allah anawapa Mitume na Manabii kwa aya mbali mbali na miujiza, ambayo Allah huipitisha katika mikono ya Mitume na Manabii wake katika mambo ambayo yanavunja mazoea ya kawaida ya kimaumbile ambazo mwanadamu hawezi kufanya, mfano wa hayo ni alama ya Musa (‘Alahyi Salaam) pale fimbo yake ilipogeuka kuwa nyoka, Allah amesema: “Na nini hicho kilichomo mkononi mwako wa kulia, ewe Musa? Akasema: Hii ni fimbo yangu; naiegemea na ninawaangushia majani kondoo na mbuzi wangu. Tena inanifaa kwa matumizi mengine. Akasema: Itupe, ewe Musa! Akaitupa. Mara ikawa nyoka anaye kwenda mbio. Akasema: Ikamate, wala usiogope! Tutairudisha hali yake ya kwanza. Na uambatishe mkono wako kwenye ubavu. Utatoka mweupe pasipo kuwa na madhara yoyote. Hiyo ni ishara nyengine. Ili tukuonyeshe baadhi ya ishara zetu kubwa. ” (20:17-23)
Na alama ya Issa (‘Alahyi Salaam) alipokuwa akiponya mbalanga na ukoma kwa idhini ya Allah, katika ndimi ya Mariam Allah amesema akimbashiria Issa: “Maryamu akasema: Mola wangu Mlezi! Vipi nitampata mwana na hali hajanigusa mwanaadamu? Mwenyezi Mungu akasema: Ndivyo vivyo hivyo, Mwenyezi Mungu huumba apendacho. Anapo hukumu jambo, huliambia: Kuwa! Likawa. Na atamfunza kuandika na Hikima na Taurati na Injili. Na ni Mtume kwa Wana wa Israili kuwaambia: Mimi nimekujieni na Ishara kutoka kwa Mola Mlezi wenu, ya kwamba nakuundieni kwa udongo kama sura ya ndege. Kisha nampuliza anakuwa ndege kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na ninawaponesha vipofu wa tangu kuzaliwa na wakoma, na ninawafufua maiti kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na ninakwambieni mnacho kila na mnacho weka akiba katika nyumba zenu. Hakika katika haya ipo Ishara kwenu ikiwi nyinyi ni wenye kuamini. Na ninasadikisha yaliyo kuwa kabla yangu katika Taurati, na ili nikuhalalishieni baadhi ya yale mlio harimishiwa, na nimekujieni na Ishara kutokana na Mola Mlezi wenu. Kwa hivyo mcheni Mwenyezi Mungu na nit’iini mimi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi na ni Mola wenu Mlezi. Basi muabudni Yeye. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka. ” (3:47-51)
Na alama kubwa kwa Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) ambayo ni Qur-aan, pamoja na yeye kutokusoma kilichoandikwa, Allah amesema: “Sema: Wangeli kusanyika watu na majini ili walete mfano wa hii Qur’ani basi hawaleti mfano wake, hata wakisaidiana wao kwa wao. Na hakika tumewaeleza watu katika hii Qur’ani kwa kila mfano. Lakini watu wengi wanakataa isipo kuwa kukanusha tu.” (17:88 -89).
Na aya nyinginezo kuhusu Mitume na Manabii.
Na kwa kufuatilia na kusoma aya na miujiza ambayo Allah Ta’ala amewapa Mitume na Manabii wake tunaona zinaingia katika mambo matatu: Elimu, uwezo na kujitosha (utajiri) hivyo basi kutoa habari kuhusu mambo ya ghaibu yaliyopita na yajayo; kama vile Issa (‘Alahyi Salaam) alivyowaambia watu wake chakula watakachokula na watakachohifadhi katika majumba yao-na Mtume wetu Muhammad kuelezea kuhusu Umma zilizotangulia na kuwajulisha kuhusu mitihani mbali mbali na dalili za Kiama ambazo zitakuja baadae–yote hayo yanatokana na elimu, na kubadilika fimbo kuwa nyoka, na kuponya mbalanga na ukoma, na kufufua watu na Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) kuepushwa na madhambi, na katika mlango wa kudura, na kumlinda kwa aliyetaka kumdhuru, Allah amesema: “Ewe Mtume! Fikisha uliyo teremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi. Na ikiwa hukufanya hayo basi hukufikisha ujumbe wake. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.” (5:67),
Mambo haya matatu: elimu, uwezo, na kujitosha (utajiri), ambayo miujiza inarejea haifai kuwa katika sura ya ukamilifu ila kwa Allah Ta’ala.
Katika dalili za ukweli wa utume ni manabii waliotangulia kutabiri kuja kwa manabii wanaofuatia, Allah amechukua ahadi na mkataba (Mithaqi) ya kila Mtume ya kuwa lau akimtuma Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasalam) katika maisha yake watamuamini, Allah Ta’ala amesema: “Na pale Mwenyezi Mungu alipo chukua ahadi kwa Manabii: Nikisha kupeni Kitabu na hikima, kisha akakujieni Mtume mwenye kusadikisha mliyo nayo, ni juu yenu mumuamini na mumsaidie. Akasema: Je, mmekiri na mmekubali kushika agizo langu juu ya hayo? Wakasema: Tumekubali. Akasema: Basi shuhudieni, na Mimi ni pamoja nanyi katika kushuhudia.” (3:81).
Manabii na Mitume walikuwa wakiishi na kuchanganyika na watu wao na kuamiliana pamoja nao; na hivyo kuwa rahisi kwa watu kujua nyendo zao, na kujua ukweli wao, hivyo basi pale walipomtuhumu Maryam na mwanae Mtume wa Allah Issa (‘Alahyi Salaam) Allah alidhihirisha ukweli wao, Allah amesema: “Akenda naye (mwanawe) kwa jamaa zake amembeba. Wakasema: Ewe Maryamu! Hakika umeleta kitu cha ajabu! Ewe dada yake Harun! Baba yako hakuwa mtu muovu, wala mama yako hakuwa kahaba. Akawaashiria (mtoto). Wakasema: Vipi tumsemeze aliye bado mdogo yumo katika mlezi? (Mtoto) akasema: Hakika mimi ni mtumwa wa Mwenyezi Mungu. Amenipa Kitabu, na amenifanya Nabii. Na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale niwapo. Na ameniusia Sala na Zaka maadamu ni hai, Na nimtendee wema mama yangu. Wala hakunifanya niwe jeuri, mwovu. ” (19:27-33).
Hivyo ndivyo Issa alivyozungumza utotoni. Makureishi walikuwa wakimuita Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) kabla ya kutimilizwa kwake kuwa ni ‘Mkweli Mwaminifu; na hiyo ni kutokana na ukweli wake na uaminifu wake, Qur-aan imeelekeza hilo; ili kutoa dalili ya ukweli wa Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) kwa sababu maisha yake binafsi yalikuwa ni dalili kubwa, Allah amesema, “Sema: Mwenyezi Mungu angeli taka nisingeli kusomeeni, wala nisingeli kujuvyeni. Kwani nalikwisha kaa nanyi umri mzima kabla yake! Basi, je! Hamzingatii? ” (10:16).
Miongoni mwa dalili za utume na kuafikiana Da’wah ya Mtume katika misingi yake pamoja na misingi ya Da’wah ya Mitume na Manabii wote, hivyo Mtume analingania kwenye Tawhid ya Allah Ta’ala: kwani hili ndilo lengo ambalo kwa ajili yake Mwenyezi Mungu ameumba na kutuma Mitume, Allah amesema: “Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimfunulia ya kwamba hapana mungu isipo kuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu. ” (21:25)
Na akasema: “Na waulize Mitume wetu tulio watuma kabla yako: Je! Tulifanya miungu mingine iabudiwe badala ya Rah’mani? ” (43:45)
Akasema: “Na kwa hakika kwa kila umma tuliutumia Mtume kwamba: Muabuduni Mwenyezi Mungu, na muepukeni Shetani. Basi kati yao wapo alio waongoa Mwenyezi Mungu. Na kati yao wapo ambao ulio wathibitikia upotovu. Basi tembeeni katika ardhi, muangalie ulikuwaje mwisho wa wanao kanusha.” (16:36)
Na katika yote haya ndio iliyokuwa da’wah ya Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) Mtume alikuwa ni sawa na wanadamu wengine ila alifadhilishwa na kukirimiwa na Wahyi, Allah amesema: “Sema: Mimi ni mwanaadamu kama nyinyi. Ninaletewa Wahyi kwamba Mungu wenu ni Mungu Mmoja. Mwenye kutaraji kukutana na Mola wake Mlezi basi naatende vitendo vyema, wala asimshirikishe yeyote katika ibada ya Mola wake Mlezi.” (18:110),
Hivyo basi hawezi kulingania ufalme au uraisi, Allah Ta’ala amesema: “Sema: Mimi sikwambiini kuwa ninazo khazina za Mwenyezi Mungu. Wala sijui mambo yaliyo fichikana. Wala sikwambiini kuwa mimi ni Malaika. Mimi sifuati ila yanayo funuliwa kwangu. Sema: Je, wanakuwa sawa, kipofu na mwenye kuona. Basi hamfikiri?” (6:50)
Wala hawawaulizi watu ujira wa
Da’wah yake atoayo Allah amezungumza akiwaelezea Mitume yake Nuuh, Huud Swalah, Luut na Shu’ayb kuwa waliwaambia kaumu yake: “Na sikutakini juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. ” (26:109) Kadhalika katika aya zifuatazo vile vile (26:127, 145, 164 na 180)
Na Muhammad akawaambia watu wake: “Sema (Ewe Mtume): Sikuombeni ujira juu ya haya, wala mimi si katika wadanganyifu. ” (38:86)
Katika dalili za ukweli wa manabii na waliotumwa vile vile ni Allah kuwanusuru na kuwahifadhi; itaingiaje akilini mtu adai utume au unabii nae ni muongo katika Da’wah yake, halafu baada ya hapo Allah atawalie kumnusuru, kumuhifadhi, kumuunga mkono na kueneza Da’wah yake, bali hilo halitoshi wala hamteremshii adhabu yake!! Allah amesema: “Wala msiseme uwongo, kwa kuropokwa na ndimi zenu: Hichi halali, na hichi haramu - mkimzulia uwongo Mwenyezi Mungu. Hakika wanao mzulia uwongo Mwenyezi Mungu hawatafanikiwa.” (16:116)
Na akasema Mtukuka, “Na lau kama angeli tuzulia baadhi ya maneno tu, Bila ya shaka tungeli mshika kwa mkono wa kulia, Kisha kwa hakika tungeli mkata mshipa mkubwa wa moyo!” (69:44 -46).