MATARAJIO MEMA

MATARAJIO MEMA

MATARAJIO MEMA

(1)

Joji alijiunga katika kundi la wanaosoma kuhusu Ukristo, alichokiangalia zaidi kwa kina ni usahihi wa Agano Jipya na la Kale na vilivyoongezwa juu yao. Alihisi kuwa alikuwa akiogopa kuangalia maudhui haya kwa sababu yalikuwa ni nyeti. Hata hivyo hapana budi kuyaangalia kwa kina; ili ahakikishe usahihi wa kitabu chake kitukufu. Ni jambo gumu kitabu kitukufu kitiliwe mashaka na sisi kudumu katika hali hiyo. Joji aliendelea kusoma hadi muda wa chakula cha mchana kilipowadia akiwa anasoma….nesi alimpitia akampima joto lake, akiwa ameshughulishwa na kusoma, nesi alimwambia:

Kana kwamba wewe ni mwanafunzi unaengojea mitihani?

Ha ha ha, ndio mimi ni mwanafunzi wa shule ya maisha, na mitihani yangu ima nifaulu; ili niwe mwenye furaha, au nifeli; ili niwe mwenye huzuni.

Unaelekea ni mwanafalsafa!

La msingi ni kupasi mitihani.

Kupasi mitihani ya maisha ni ngumu, watu wengi kwa bahati mbaya wanafeli.

Kwanini?

Kwa sababu wenyewe wanataka kufeli, wala hawataki kufaulu.

Ima wewe unafanya falsafa au unakwenda kinyume na ukweli wa mambo kwa njia ya ajabu.

Bali ni kweli nafanya falsafa, je utaniruhusu niondoke kwani nina kazi.

Joji alitabasamu kwa mshangao akishangazwa na mazungumzo yake mwenyewe, jinsi gani alivyojirusha kwenye falsafa ya kina kabisa, kisha akamaliza mazungumzo yake na kuondoka upesi….”Nini maana ya watu wengi kupenda kuanguka kwenye mitihani yao maishani” Je inaingia akilini?! Kwa hali yoyote ile yupo nae hospitalini, na atamuulizia hilo muda atakapoonana naye.
Tom aliingia chumbani kwa Joji akiwa amezama kusoma. Joji hakutanabahi kuingia kwake, hadi aliposimama pembeni yake na kumgusa mabegani huku akitabasamu……

Lazima utakuwa umeufahamu Ukristo pamoja na madhehebu yake mbali mbali.

Tom –Karibu sana.

Vipi hali yako leo hii?

Vizuri, kama unavyoniona, sikutarajia kama utafika leo.

Nimechagua muda ambao hakuna anayeweza kudhania kama nitakuja kwako na Katarina hayupo.

Kwa nini?

Nahisi kuwa nimekosea kumbusu, na sijui kwa nini nilifanya vile, na nahisi kuwa hutopendezwa nikimbusu, kama ambavyo hutoniamini ninayokuambia, una haki zote kufikiri hivyo.

Joji alitabasamu na kusema:

Hilo jambo ni dogo, lakini kwa nini umemwambia Baraad kuwa unampenda Katarina na kuwa unambusu kila mara, na una starehe naye?

Mimi nimesema hivyo?

Haya ndiyo anayosema mkuu wa ofisi yako “Baraad” alipokuja kunitembelea leo hii.

Hukuniamini hapo zamani vipi utaweza kuniamini leo hii? Yeye ni muongo kabisa na mwenye kutia aibu.

Unayemzungumzia ni mkuu wa ofisi yako, na siku ile asubuhi aliniambia akiwemo Katarina, je hukumwambia vile vile kuwa nitakwenda Tora bora? Je alibuni kuwa tulizungumza mambo haya?

Ah ah, nitalazimika sasa kukueleza baadhi ya mambo ambayo sikutaka kufanya hivyo.

Haya niambie.

Nilikuwa najua kuwa Baraad ambae ni mkuu wa ofisi yangu ni sekretari mbaya na asiyekuwa na maadili mazuri, lakini nilimnyamazia kwa sababu alikuwa akinisaidia pindi nilipokuwa nacheza na wanawake hapo kabla. Niamini kuwa tokea uanze kunitembelea hospitalini nimeanza kubadilika na sijui kwa nini? Na tokea hapo nikawa makini kusoma, kutafiti, na kujadiliana katika mambo ya dini na yanayoleta furaha. Hili halikumpendeza Baraad na mara nyingi aliniambia hivyo, bali alinitishia na picha za baadhi ya wagonjwa wangu wa zamani alizokuwa nazo…kisha baada ya muda nikagundua kuwa ameweka kamera akinichunguza na kuchukua sauti ndani ya ofisi yangu. Hivyo basi kwa njia hii anapiga picha na kunasa sauti na pia mawasiliano yangu yote yanayoendelea katika Kliniki. Yote haya nimeyafahamu siku tatu tu zilizopita na ilitokea purukushani nguo kuchanika katika maudhui haya na nikamtishia kumfukuza, nae akanitishia kusambaza picha zangu, na yote aliyorikodi ambayo yapo katika website moja kwa moja, na hii maana yake ni kufutiwa leseni yangu kama daktari. Na sijui cha kufanya kwa sasa. Je utaamini niliyokuambia sasa? Kama hutoamini unasamehewa kwa hilo.

Pamoja na kuwa inaonekana kuwa ni kisa cha kufikirika lakini kwa kiasi kikubwa nina ushahidi wa kuyaamini.

Ushahidi gani?

Mara ya mwisho nilipokuja kwako nilipotoka tu Baraad alinikabili, na kuniambia kuhusu Tora bora, na mimi nina hakika kuwa hukuondoka ofisini kwako muda ule na yeye hakuingia kwako.

Kwa nini hukuniambia?

Nilishangazwa sana na hali hiyo nikajisemesha: Huenda ulikuwa ni mpango wenu wa pamoja au jambo mnaloliita telepathia.

Niamini nilishakuambia ukweli kamili, maamuzi ni yako.

Nesi aligonga mlango na kuingia upesi…

Samahani kuwakatisha, daktari anataka kuongea nawe haraka, anakuja sasa hivi.

Aingie, kuna jambo gani?

Daktari akaingia….

Samahani Joji kwa ziara ya ghafla lakini jambo lenyewe ni la haraka.

Ndio daktari.

Vipimo vyote vilivyobakia matokeo yake yametoka muda si mrefu, na wewe unahitaji kufanyiwa operesheni haraka iwezekanavyo, kesho muda kama huu.

Inaelekea jambo hili ni la hatari.

Ukweli nalazimika kukuambia ndio, na ndio maana nimekuja wakati huu, unao muda wa kufikiria, na kusaini uthibitisho wa kuafiki kwako kabla ya saa sita mchana hapo kesho.

Kufikiri na kusaini…na kuthibitisha!

Inapasa nikuelezee kwa urefu na uwazi, virusi ambavyo vinapandisha joto lako tumevigundua kuwa vinaharibu sehemu ya ubongo wako kila muda ambapo joto lako linapopanda, na hilo linaweza kutokea tena kesho saa mbili usiku, na hiyo ina maana ya kuwa halitokujia hilo ila tutakapokuwa tumeanza operesheni, kufaulu kwa opresheni hii ni asilimia 60 tu kwa bahati mbaya.

Na hiyo asilimia 40 iliyobakia?!

Inaweza kutokea uharibifu katika baadhi za sehemu ya ubongo wako.

Hilo lina maana gani?

Samahani siwezi kulitabiri hilo kwa sasa… inaweza isitokee chochote, na yanaweza kuingia mambo mengine.

Kinachotakiwa sasa kwangu ni kuwafiki na kusaini uthibitisho wa hilo!

Ndio.

Kama sitoafiki itakuwaje?

Itabidi usaini uthibitisho kuwa ulitakiwa kufanya hivyo ukakataa pamoja na kuwa kwa dhana yangu ni kuwa operesheni ni bora zaidi kwako, pamoja na kuwa kadhia hii ni nzito kwetu, je una swali lingine?

Hapana, isipokuwa kama kutajitokeza habari mpya muhimu katika jambo hili.

Hapana jingine, kwa ujumla sijazungumza nawe ila baada ya kuongea na timu ya madaktari na hii ndio rai yao wote, kama utakuwa na swali wakati mwingine, unaweza kumuuliza nesi, naye atawasiliana nami moja kwa moja ili nijibu swali lako lolote lile, na natarajia utapata muda wa kufikiria na kusaini uthibitisho kabla ya saa sita mchana.

Nitafikiri na kushauri na kukujibu.

Chukulia jambo hili kwa wepesi na hali ya kawaida bila ya khofu kama ulivyonizoesha; maisha, mauti na maradhi ni maumbo mbali mbali ya nafsi ya mwanadamu katika maisha yake ya kila siku, inapasa kuishi na hali hizo, nakuomba ruhusa nitakuja asubuhi saa tatu kukuona, na kama utakuwa na jambo la kuuliza kabla ya hapo mwambie nesi, anipigie.

Asante.

Daktari aliondoka na Joji alipigwa na ukimya hadi alipokatwa na sauti ya Tom…

Joji…maisha hayana maana kama mtu hatokuwa katika furaha, kama ambavyo mauti hayana maana kama hatutoamini ufufuo na hesabu, kitu cha ajabu falsafa ya mauti na uhai!

Bali cha ajabu ni falsafa ya kuwepo kwetu! Kwa nini tumeumbwa? Na tunaelekea wapi!

Kama ni hivyo unafikiria nini?!

Nilikuwa nafikiria: Je mimi nataka maisha au mauti?

Haihitaji kufikiri, hakuna asiyetaka maisha.

Kwa nini basi kujinyonga? Je sio kweli kwamba idadi ya watu wanaotaka kujinyonga inaongezeka duniani kote? Nami siku moja si nilikuwa natamani kujinyonga?

Ajabu ya jambo hili kwako, mwenye kujinyonga anamaliza huzuni yake kwa huzuni, ama mtu mwenye furaha hahitaji kufanya hivyo kamwe.

Nilipokwenda kutaka kujinyonga dunia yote ikawa dhiki kwangu juu ya upana wake, na nilikuwa katika huzuni kubwa mpaka nikawa nataka kuondosha huzuni yangu kwa huzuni kama ulivyosema.

Kwani bado upo kwenye huzuni, ili ufikirie kama unahitaji mauti au uhai?

Ukweli ni kuwa tokea nianze safari yangu ya njia ya furaha nami nahisi furaha na huwa naiambia nafsi yangu. Vipi nitakapofikia furaha itakuwaje?

Kama ni hivyo shikamana na uhai ili upate furaha.

Mimi nahitaji uhai, lakini swali ni kwamba: Je uhai unanihitajia? Nimemuona Maria akipigana akitaka maisha, lakini mauti yalimpiga mweleka…..

Mtumainie Mungu atakusaidia.

Ha ha ha inaelekea sasa wewe ni mwenye kujiamini, mwenye dini ewe Tom!

Je si kukuambia kuwa nimebadilika? Niamini sikutarajia kubadilika, bali sijapanga kufanya hilo, na sijui kwa nini nimebadilika lakini ninakuambia ni kweli nimebadilika.

Pamoja na hali niliyokuwa nayo, lakini nina swali: Je ulikuwa ni mwenye furaha zaidi hapo kabla au sasa?

Naweza kujibu swali lako ulilonitumia kwenye barua pepe hapo kabla kuhusu starehe ya kiwiliwili na kiroho, nilikuwa ninafurahisha kiwiliwili changu kwa huzuni ya roho yangu, na hivyo basi kiwiliwili changu kinaumia hali kadhalika.

Na sasa hivi?

Sijafikia kwenye hiyo furaha bado, lakini siko katika ile hali ya huzuni kama ilivyokuwa kabla.

Je ungekuwa katika nafasi yangu ungetamani mauti au uhai?

Uhai bila ya shaka, kama ungeniuliza hapo kabla ningekuambia natamani mauti…huzuni ya mauti huisha kwa huzuni ya uhai.

Nakumbuka pindi nilipokutana na kikongwe njiani nikienda kujinyonga, alikuwa ni mtu mwenye furaha sana, alikuwa akicheza na wajukuu zake, laiti ningechukua anuani yake.

La muhimu kwa sasa, ni kusaini uthibitisho wa kukubali operesheni, madaktari wanajua zaidi kuliko sisi ila nakushauri umshauri Katarina kwanza.

Na hii ndio rai yangu vile vile…pamoja na kuwa ni lazima kupanga mambo yangu. Nafasi ya kufeli operesheni hii ni asilimia 40.

Kuwa na matumaini rafiki yangu na haiwi ila unachokipenda, na si vibaya mmoja wetu akajitayarisha na chochote kinachoweza kutokea, utasimama kutoka kwenye maradhi yako na utafikia furaha hata hivyo usisahau kunichukua, nitakuacha ufikiri katika maudhui haya na nitakuja kesho kukujulia hali yako.

Joji alijilaza akitafakari maana ya mauti ambayo huenda yakamfika, mauti ambayo yalimfika Maria mwanae wa kike mbele ya macho yake. Mauti yana maana gani? Bali maisha yana maana gani? Je mauti ni raha au suluhiho la matatizo ya dunia? Au ni mwisho wa furaha duniani? Ikiwa jibu ni hilo la mwanzo basi bora mauti, na ikiwa ni hili la pili hii ina maana kuwa amekwisha fikia kwenye furaha na ameshaifahamu, alitabasamu kwa dhihaka akiwa anafikiria kwa njia hii, na akajisemesha: Inaelekea kuwa nitakufa huku nikiendelea na falsafa ambayo haitonifikisha popote.
Fikra zake zilikatwa na sauti ya simu ikilia, akiangalia ilikuwa ni Adam…

Hallo.

Ndio Joji nilipenda kujua maendeleo yako na vipi afya yako?

Nipo baina ya uhai na umauti, sijui katika hayo iliyo karibu na mimi?

Sijakufahamu bado, kwani vipi?

Asilimia 60 ya maisha na 40 ya mauti au kilema.

Sijafahamu kitu, kama unatania mimi sipendi utani wa namna hii.

Laiti ningekuwa nafanya utani, lakini huu ni ukweli… huenda kesho nikafanyiwa operesheni na uwezekano wa kufaulu ni asilimia 60.

Tunamshukuru Mungu kwa hali zote.

Kiasi gani natamani kukuona leo.

Leo tena haiwezekani; muda wa kutembelea wagonjwa umekwisha, kwa nini hukuwasiliana nami mapema?

Sijui, je unaweza kuja kunitembelea katika muda wa kutembelea wagonjwa kesho asubuhi?

Bila ya shaka nitakuja, lau ningeweza kuja sasa hivi ningekuja, lakini nakuhakikishia kuwa umri wa watu upo katika mikono ya Mungu na sio katika mikono ya madaktari pamoja ya kuwa wao ndio sababu muhimu.

Sijui; je nayaogopea mauti au nipo tofauti? ambacho ninakifahamu ni kuwa umauti ni ukweli ulio mpana ambao unarejea upya utaratibu wa maisha kwa ukamilifu.

Usihofu, wala usitishike; Mungu hutuhurumia sisi zaidi kuliko hata nafsi zetu.

Niamini sijui, ninaogopa au nina wasiwasi? Au nina nini? Ninachokihisi ni kuwa ni lazima niyapangilie maisha yangu kwa mara nyingine, unaona dharau yangu kwangu mwenyewe?

Dharau gani?

Ninapoogopea maisha nimeamua kuyapanga maisha yangu upya, je haikuwa vizuri kufanya hayo hapo kabla nilipokuwa nayapupia, na sio wakati huu tena ambapo nipo nje yake?

Hata hapo kabla ulijitahidi kuyapanga, na kwa hali hiyo inabidi uyapange yaliyobakia, hata hivyo hayo yaliyobakia anayafahamu Mungu pekee….na mimi napenda matarajio mema na nachukizwa kabisa na tabia ya mtu kukosa rajua.

Kwa hakika nipo katika kukanganyikiwa, je unatarajia kuwa nitakufa?

Utaishi apendapo Mungu, na utabakia hadi upate furaha uitafutayo katika njia yake, na wakati huo ndipo utakapoona maana ya maisha haya ya duniani na ya baada ya mauti.

Maelezo mazuri, “Maisha yetu baada ya mauti”, hili nitajadiliana nawe kesho, samahani ninalazimika kumpigia Katarina nimjulishe.

Ndio…. Ni lazima ushauriane na mke wako, samahani kama nimrefusha mazungumzo, na kuaga kwa jina la Mungu, kwa heri.

Ni kiasi gani nakushukuru Adam, nitakusubiri kesho, kwa heri.

Joji alimaliza mazungumzo yake na maneno ya Adam yakiendelea kugonga kichwa chake, alijikuta akikariri maneno yale bila kujijua: “Umri wetu upo katika mikono ya Mungu na si katika mikono ya madaktari. “Mungu anatuhurumia zaidi kuliko hata nafsi zetu. “Napenda matarajio mema na sipendi dege baya,” “Tunapokuwa wenye furaha, maisha yetu ya duniani na maisha yetu baada ya umauti yanapata maana….” Hakufahamu kwa nini maneno ya Adam ya kawaida lakini ya kina yanatingisha nafsi yake kila mara? Je siri ipo kwenye maneno yenyewe au kwenye ukweli wa Adam mwenyewe? Au ni kwa sababu amekanganyikiwa na hawezi kuitawala nafsi yake.
Joji alikatishwa na mtiririko wa fikra zake, ni lazima ampigie Katarina na kumjulisha ili apate ushauri wake.

Hallo Katarina, nimekutamani sasa na nilikuwa nakusubiria leo hii.

Nilikuwa nakuja kwako isipokuwa jambo dogo limenichelewesha.

Salama lakini!

Sali alikuwa na kazi za nyumbani alizopewa shuleni na akaomba msaada wangu.

Uko wapi sasa?

Nyumbani, kuna nini Joji?

Nilikuwa nataka kukushauri katika jambo tu; daktari ameniambia kuwa naweza kufanyiwa operesheni kesho kama nitakubali.

Kesho, haraka hivyo? Ni operesheni ya nini?

Alichoniambia ni kuwa ni bora kufanya operesheni kesho saa mbili usiku.

Mpenzi wangu, unasema nini? Ninakuja sasa hivi hospitalini.

Nadhani ni bora uje kesho asubuhi.

Ni operesheni ya nini?

Operesheni ya kichwa.

Kichwa!!! Je ni ya hatari?

Huenda ikawa hivyo, cha msingi ni kuwa daktari ameniambia kuwa bora ifanyike pamoja nakuwa uwezekano wa kufanikiwa ni asilimia sitini tu, na nini rai yako?

Sijui, nitasali kwa ajili yako usiku wote, na asubuhi nitakuja na Maiko na Sali.

Nitakusubiri mpenzi wangu, kwa heri!

Katarina alijitupa kitandani pake na kulia kilio kikubwa hakuweza kuvumilia kufikiria kutoweka kwa Joji kutoka katika maisha yake…itakuwaje kama operesheni itafeli… itakuwaje kama atakuwa mlemavu…vipi na vipi……? Kisha akasimama akiomba na kumsalia Joji…..
Ama kwa upande wa Joji fikra zake zilihamia kwa Katarina na watoto wake, na sehemu kubwa ya fikra hizi zilikuwa kuhusu mali zake, alitabasamu huku akikumbuka kuwa amejadidisha bima yake ya maisha; kinachomaanisha kuwa fedha nyingi zitakwenda kwa Katarina na wanawe….Kama ilivyo katika mkataba wa shirika lake utampa fedha nyingi, haswa ya kuwa alipata maradhi akiwa katika safari ya kikazi na hilo anaweza kulithibitisha. Shaka yake ipo kama Kakhi atampa chochote atakapokufa, kwani Kakhi hafikiri chochote isipokuwa katika nafsi yake tu, katika hali hiyo ya fikra mbali mbali mara lepe la usingizi likamchukuwa.

(2)

Joji aliamka mapema, alipata kifungua kinywa huku akihisi kichwa kizito kwa fikra na mawimbi ya maswali, ambapo mwishoni alikubali afanyiwe operesheni, hata hivyo hofu ilimtawala….anatakiwa afanye nini kabla ya operesheni… Katarina na wanawe hakuwasahau katika mawazo yake….
Muda wa kutembelea wagonjwa ulipoanza asubuhi ile mara Adam akawa ameshaingia chumbani akiwa na tabasamu.

Nipe habari nzuri, vipi afya yako?

Nzuri...hakuna mpya, namsubiria daktari, nataraji atafika hivi punde, pamoja na kuwa bado sina kitu.

Swadakta, si kwa uwezo wa daktari kufanya kitu, bali wanadamu wote hawawezi kufanya kitu.

Hivyo ni nani mwenye uwezo wa amri yake kwa kila kitu?!!

Mungu ndiye mwenye kumiliki kila kitu.

Ni yupi mungu wako Adam?

Mungu wangu ndio Mungu wako na walimwengu wote, achana na hili kwanza.

Kama ni hivyo wewe ni Protestant?!

Utakapofika kwenye furaha katika mradi wako wa furaha, nitakuwa pamoja nawe.

Hili linategemea kama nitaishi baada ya operesheni.

Kuwa ni mwenye matumaini mazuri …tarajia mema, ni kiasi gani nachukia mtu aliyekosa rajua.

Dunia yote imesimama juu ya matarajio mabaya, kwa nini unakataa?

Hapana dunia imesimamia matumaini mazuri, achana na ushirikina.

Kweli….Je huna hisia mbaya na namba kumi na tatu?

Hapana kabisa, sina. Mwenye kuongoza ulimwengu ni Mungu tu, kwa mnasaba huo huo ni kuwa Wachina wana hisia nzuri sana na namba kumi na tatu; Kwa sababu makato yake ya sauti yanafanana pamoja na maana ‘Lazima niishi’, hivyo jambo halifai kuwa ni la kishirikina juu ya ushirikina, na kuwa mbali na mfumo wa Mwenyezi Mungu.

Kwa kuwa wewe ni Protestant usiwe na hisia mbaya na tarehe kumi na tatu (13), hata ikiwa itawafikiana na siku ya Ijumaa? Je hujui kuwa katika historia ya masiya, kikao chake cha mwisho cha siri kilimkutanisha na wanafunzi wake, kabla ya Yahudha hajamfanyia hiana na kutaja alipojificha, siku hiyo ilikuwa ni Ijumaa na idadi ya waliohudhuria ilikuwa ni watu kumi na tatu.

Siamini ushirikina, nimekuja kukujulia hali sio kujadiliana nawe kuhusu matumaini au kukosa rajua, na napenda rafiki yangu aishi daima akiwa na matarajio mema.

Unatarajia vipi niwe na matumaini wakati uwezekano wa kufaulu operesheni ni asilimia sitini tu?!

Mungu wetu ni mwenye huruma na mkarimu, nae katika mikono yake anamiliki kila kitu, madaktari ni sababu ya hayo tu, ukitarajia mema utakuwa ni mwenye furaha tele, na inawezekana ukaishi katika hali bora zaidi, na hata asilimia ya kufaulu operesheni ni nzuri. Ama ukitarajia mabaya hali yako itakuwa mbaya, na halitokufika na kukupata isipokuwa alichokuandikia Mungu mrahimu kwako, una nini Joji kwani hauko hivi?

Nilitaka kukuambia hivi nione utasema nini, hata hivyo mimi nachukia ushirikina na udajali na najifunza kwako mapenzi ya kutaraji mema…lakini niambie: Itakuwaje mtu aliyekuwa na mfano wa hali yangu akataraji mema?

Katarina akiwa pamoja na Sali na Maiko walifika na kuingia chumbani kwa hamu sana na haraka hadi kitandani kwa Joji.

Vipi Joji usijali, hali yako vipi sasa?

Baba vipi hali yako, tunakuhofia!

Baba una nini?

Hayo yalimuathiri Adam na kumfanya aondoke aiwachie familia fursa ya kukaa pamoja na baba yao kabla ya muda wa operesheni….

Nitaomba ruhusa ya kuondoka, na samahani kwa usumbufu.

Oh Adam, samahani sikutanabahi uwepo wako.

Hapana, hapana usiondoke, nataka ubakie, labda kama una haraka.

Sina haraka, lakini sipendi kuwakera.

Hakuna usumbufu wowote ule, tutafurahi kuwepo kwako….

Joji aliwasogeza karibu Maiko na Sali na akawakalisha pembeni kitandani… nae akiwauliza kuhusu habari za shule na nyumbani….

Hali zetu nzuri baba, lini utarudi nyumbani?

Mama ametuambia utarudi baada ya siku tatu na baada ya hapo tutasafiri pamoja kwenda Roma.

Nimeshanunua tiketi, safari yetu ni baada ya siku kumi.

Umenunua tiketi?! Kwa nini? Sidhani kama hali yangu itaniruhusu.

Usihofu, utakuwa katika hali nzuri.

Nini rai yako Adam?

Maamuzi yaliyobarikiwa, na yatakuwa kwa uwezo wa Mungu….na hili ndilo jibu la swali lako.

Swali gani?

Hukuwa unaniuliza: Unatarajia vipi mema katika hali kama hii?

Kumuachia mambo yetu Mungu ambaye ni Mwenye huruma sana na mkarimu hutufanya tujihisi raha katika maisha yetu.

Katarina akizuia machozi machoni mwake: Usiku mzima nilikuwa nalia na kusali kwa ajili yako, kisha nikaona kulia kwangu hakutonufaisha, lakini dua zangu ndizo zingeweza kukusaidia, na nimechelewa kidogo ili nithibitishe safari yetu leo asubuhi, unaonaje Joji?

Ni mwenye furaha sana kwa ajili yako Katarina, sawa

tumekubaliana….Sali mtoto mzuri niambie: Je umehamasika kwenda Roma?

Sana baba, nataka kuona Trevi Fountain.

Ni ipi hiyo chemchem ya Trevi?

Ni chemchem kubwa, tulijifunza kwenye somo la Jiografia.

Na mimi nataka kuona ngome ya Saint Angelo, ni ngome, iliyojengwa kwa majivu ya wafalme, ambayo baadae ikawa makumbusho, kama tulivyosoma katika somo la Jiografia.

Ama mimi nataka kutembelea Cathedral ya Mtakatifu Patrick.

Inaelekea mambo yote yamepangwa vizuri…nataraji yote yatafanikiwa.

Watoto wale wawili walipiga makelele kwa furaha, walimbusu baba yao…. Wakati huo Adam alikuwa amekaa pembeni chumbani, akiwapa fursa kuzungumzia mambo yao ya safari kwa hamasa na furaha…na mwisho Katarina akawaambia wanawe:

Sasa hivi ni saa tatu, dereva yupo nje anawasubiri.

Vizuri ….kwa heri baba!

Kwa herini wapenzi wangu……

Joji alimgeukia Adam aliyekaa peke yake.

Samahani Adam, je hukujihisi mwenye dhiki?

Na kitu gani?

Safari yetu ya Roma; Wewe ni Mprotestant na sio Mkatoliki.

Hapana kabisa, bali nakuhimiza, ili upate kujua Ukristo kwa pande zote mbali mbali.

Wewe ni mtu wa ajabu Adam.

Muda ambao tutakuwa wakweli katika utafiti wetu kuhusu njia ya furaha, basi juhudi zetu zote na maarifa yoyote ya zaidi itatung’arishia zaidi nia yetu, inatupasa tulichunge hilo. Je sikukuhamasisha kwenda India na Jerusalem hapo kabla? Je, baada ya hapo kuna mpya gani?

Kilichokuwa kipya ni kuwa sisi na Wakatoliki tuna vita vikubwa na kisasi… Je wewe Mprotestant hukuwaua miongoni mwao mamilioni katika vita vya miaka thelathini?

Mauaji ya namna hii hayapendi yeyote, kisha ni nani aliyekuambia kuwa mimi ni Mprotestant? Huenda nikawa Mkatoliki? Utakaporudi kutoka safari yako nitakujulisha.

Inaelekea wewe ni Mkatoliki, kuna nukta ambazo mnakutana na Katarina… Nitaujua Ukatoliki katika masomo yangu siku hizi na katika safari yangu, hata hivyo hisia yangu ya mwanzo ni kuwa Ukatoliki una Upagani mwingi, nami sipendi makanisa yake ambayo yamejaa masanamu na picha mbali mbali utadhani ni mahekalu ya wapagani.

Na unapenda Uprotestant ambao unaua watu?!

Hili ndilo ambalo linanithibitishia sasa kuwa wewe ni Mkatoliki.

Haya sio makusudio yangu, katika utafiti wako katika njia ya furaha, tafuta haki popote iwapo na dhehebu lolote, na wakati huo utapata furaha, raha na tumaini.

Katarina alirejea chumbani baada ya kuwasindikiza wanae.

Naomba msamaha kwa kuchelewa, Maiko na Sali walitaka niwachukulie Juisi na sandwitches kabla ya kwenda kwa dereva.

Nakushukuru Katarina kwa mpangilio huu wa safari, nafsi yangu ilishaondosha hofu ya mauti yaliyokuwa yananinyemelea.

Pindi roho ya mwanadamu inapopaa, na hakika zinapodhihirika mbele yake, na kujua kuwa mauti hayamkwepi, na yakuwa yanaweza kumfika muda wowote basi mtu huyu hawezi kuwa mtumwa wa matamanio ya maisha na starehe zake, na hayamuathiri mtu huyo yaliyomo duniani; kuathiri akili yake na hamu zake. Mtu anayejitambua na kutambua maana ya uwepo wake anaweza kwa kutumia matarajio yake kufahamu kwa wepesi kuwa anaishi ili afe, na ya kuwa anakufa ili aishi milele, baada ya hapo.

Falsafa nzuri kabisa, tunaishi ili tufe, na tunakufa ili tuishi, lakini tatizo lipo kwenye maumivu ya umauti.

Yesu alivumilia maumivu kwa ajili ya mwanadamu, maumivu ni kipengele cha msingi katika kumuokoa milele, na kuvumilia kwetu maumivu ni dalili kuwa tunampenda Masiya.

Kama ni hivyo basi dunia ni ya nini?

Faida ya kuwepo duniani ni kutumia muda wako katika kumtumikia Bwana na kumhudumia Bwana tu.

Nini rai yako Adam?

Katika nini?

Ya kuwa maisha yetu yote yawe katika kumuhudumia Bwana na kutafuta radhi zake.

Nakubaliana kabisa na hilo…isipokuwa kumhudumia Bwana sio katika sala peke yake.

Katarina kwa mshangao:

Vizuri sana, mara nyingi tunasahau –kwa bahati mbaya hata mapadri –kuwa maisha yote ni ibada ambayo yanapasa kuwa kwa Mungu.

Joji kwa tabasamu la dhihaka.

Swali linalobakia ambalo linakariri mara kwa mara ni nani anayemuabudu Mungu mwenye huruma haswa? Na ni nani anayemwabudu sanamu, na kuliita kuwa ni Mola wake? Mungu wake?

Adam kwa himizo:

Huenda swali hili likawa ndilo swali la hatari zaidi katika historia.

Joji unakusudia tofauti iliyopo baina yetu kuhusu Mungu.

Unakusudia nini?

Sisi Wakristo tunakubaliana kuwa Mungu yupo katika nafsi tatu, na wamekubalia kuwa ya kwanza katika hizi tatu ni Bwana, na ya pili ni Mwana, na ya tatu ni Roho Mtakatifu, na wote watatu ni Mungu mmoja……hata kama baada ya hapo tutatofautiana kuhusu tabia ya mwana na roho mtakatifu.

Sijakusudia hilo wala haikuniingia akilini, na jaribu kufikiria hilo, ambalo sikufahamu ni kuwa vipi watatu watakuwa mmoja, na mmoja watatu, wapo sawa sawa katika kiini tofauti, katika sifa na katika tabia, na pamoja na hayo yote ni Miungu!

Hili ni moja katika kadhia kubwa na nzito katika Ukristo, na shauri hili tulizungumzie huko Roma, ni maudhui magumu ambayo hatuwezi kuyazungumza sehemu kama hii.

Hamna neno, pamoja na kuwa mimi hali kadhalika sifahamu ni jinsi gani Mungu ambaye maisha yetu yapo kwa ajili yake hatumjui vizuri bali ni vigumu kumfahamu. Wakati mwingine sioni tofauti baina yetu na wapagani!!

Niamini, sikimbii mjadala, hili ni tatizo la kila Mkristo, vyovyote awavyo madhehebu yake, hivyo ni vizuri tuyajadili kwa kina tukiwa Roma.

Adam akitabasamu:

Mimi nakubaliana na Katarina, haya ni maudhui ya hatari yenye utata, ni katika maudhui muhimu sana, wala haifai kuyajadili haraka haraka kwa njia hii, kwani mwenye akili hawezi kuendelea katika dini anayoiona mwenyewe kuwa ni ya kipagani, wala haiwezekani katika dini za mbinguni ikawa ni ya kipagani.

Ha ha ha, na mimi vile vile nakubaliana nanyi Wakatoliki wawili, pamoja na kuwa ninaamini kuwa kila Mkristo anahisi upagani wakati mwingine.

Katarina kwa mshangao.

Je wewe ni Mkatoliki ewe Adam?

Wakati mwingine huniita Mkatoliki na wakati mwingine huniita Protestant.

Ha ha ha, nimehakikisha sasa kuwa ni Mkatoliki…..

Daktari aliingia chumbani akimkuta Joji akicheka…… alikaribia kitandani mwa Joji na kusema:

Nilikuwa nina hakika nitakukuta mwenye furaha kama hivi pamoja na niliyokuambia.

Karibu, kwa nini ulikuwa na hakika kiasi hiki?

Msomi yeyote na mtu mwenye dini ni lazima atakuwa ni mwenye kujisalimisha zaidi kwa Mungu kuliko mwingine yeyote.

Lakini Mungu ni nani?

Nilikuambia hapo kabla kuwa wewe ni mwanafalsafa, mimi ni Mkristo na nakwepa maudhui haya; mimi siyafahamu pamoja na jitihada kubwa niliyofanya kuhusu hilo, lakini ni mwenye hakika ya kuwepo Mungu, mwenye huruma, mkarimu na mwenye uwezo na hili mimi linanitosha…

Lakini mimi sihisi kama inanitosha kabisa, iweje nimuabudu nisiyemfahamu?

Wewe unafanya falsafa, cha msingi je umesha saini uthibitisho wa kufanya operesheni?

Hapana, lakini ipo tayari kwa kusainiwa, au sivyo Katarina?

Je kuna uwezekano mwingine wa kufaulu kwa operesheni?

Kuna hospitali Ujerumani ambayo ni bora zaidi kwa operesheni hii, lakini kwa hali zote haiwezekani kukuhamisha hospitali nyingine yoyote, operesheni hii inapaswa kufanywa leo hii. Jana tumewasiliana na mshauri wetu aliyepo Ujerumani na akatupa matumaini makubwa, ama uwezekano wa kuzidi asilimia kufaulu operesheni sijui chochote kipya.

Sasa unatunasihi nini?

Kusaini uthibitisho haraka, tutaanza uchunguzi wa awali kwa ajili ya operesheni saa mbili usiku.

Nani atakayefanya operesheni hii?

Mkuu wa upasuaji Dr. Steve Maiko, yeye daktari mtaalamu mshauri.

Unaweza kutupatia karatasi za kusaini, kama kuna jambo lingine la kutunasihi ni vizuri.

Hamna, ila ningependa uendeelee kuwa katika hali ya furaha hadi operesheni, katika majaribio yangu ambayo sio rasmi ni kuwa nafsi ya mtu mwenye matumaini huwa ni mwenye mafanikio zaidi katika operesheni yake.

Vizuri…..huenda ikawa unaafikiana na Adam kuhusu matarajio mema.

Nadhani ya kuwa watu wote wenye akili wanakubaliana katika hilo ukiwemo wewe vile vile.

Bali huenda Katarina ametushinda sote kwa kututayarishia tiketi ya safari baada ya operesheni.

Vizuri sana wewe huhitaji baada ya operesheni zaidi ya wiki moja ya mapumziko na kwa ajili ya kufuatilia hali yako, kisha baada ya hapo unaweza kuondoka. Pamoja na kua tunashauri kutosafiri ila baada ya siku kumi baada ya operesheni.

Tunamshukuru Mungu, baada ya siku kumi kutokea sasa hivi, nadhania nimekadiria vizuri tarehe za safari.

Ndio, hili ni jambo zuri kwako… Unajua Joji nakupa hongera kwa kuwa na mke na marafiki zako wazuri. Karatasi za uthibitisho zitafika muda sio mrefu ili uzisaini, na tutaanza matayarisho ya operesheni, nakutakia mafanikio katika afya yako.

Baada ya daktari kuondoka, Joji alimgeukia Katarina na kusema…

Tunaelekea kufanya operesheni, na sina muda mrefu kabla ya operesheni, nataka kuweka vizuri mambo yangu.

Vizuri, unakusudia nini?

Nimeandika maelezo ya mali zote ninazomiliki ili zisipotee baada ya kufa kwangu, na zote nimeziandika kwako na kwa wanangu tu.

Usiseme hivyo Joji….utaishi na utaamka salama.

Samahani kukukatisha, pamoja na matarajio mema niliyokuwa nayo nakuthibitisha kuwa utatoka salama, jambo hili ni muhimu sana; na kama hutofanya hivyo huenda baadhi ya mali zako zikapotea. Na pia huenda ukamzuia mkeo na haki zake kama kweli baadhi ya mitazamo ya kanisa itafanyiwa kazi.

Sikufahamu, unasemaje! hivyo na wewe ni mtu mwenye dini?

Vipi kuhusu baba yako na mama yako?

Sijawaona yapata miaka kumi.

Huenda ikawa huu si wakati wake…. Lakini hili ni kosa bila shaka.

Naafikiana nawe, nimezungumza nao zaidi ya mara moja, natamani kama wangekuwepo.

Inaelekea leo hii mnaafikiana nami, ninawaahidi nikizinduka baada ya operesheni nitakwenda kuwatembelea kabla ya safari yangu… Inaelekea operesheni itakuwa ni mwisho wa maisha yangu.

Lau kama utawaashiria katika wasia wako itakuwa ni kheri zaidi.

Ndio, kitabu kitakatifu kimeusia kuhusu wazazi wawili: Hakika Mwenyezi Mungu ameusia akisema: “Mkirimu baba yako na mama Yako.”

Kwa bahati mbaya wasia katika kitabu kitakatifu wakati mwingine unagongana, kwa mfano nimesoma unachosema na nimesoma vile vile: “Ikiwa mmoja anakuja kwangu wala hambughudhi baba yake au mama yake au mke wake au watoto wake na ndugu zake au hata nafasi yake, basi mtu huyu nafasi kuwa mwanafunzi wangu.”

Katika Ukatoliki kukiwepo na mgongano katika akili zetu kama ulivyotaja, basi maudhui hayo hupelekewa Papa ili kukata maamuzi, ama Waprotestant wanataabika sana katika hilo.

Mtaturejeshea Upapa unaochukiza, unaoondosha akili; cha msingi, tutajadili hili baadae. La msingi turudi pale tulipokuwepo, nitawaongeza wazazi wangu katika usia, kulingana na wasia wenu, na mtakuwa ni mashahidi wa usia huu baada ya muda kidogo.

Hili ni jambo muhimu, pamoja na uhakika wangu kuwa utatoka salama kwa ruhusa ya Mungu.

Kadhalika nimeifanyia upya bima ya maisha yangu kabla ya mwezi mmoja hivi, na hili vile vile ni dhamana yenu baada ya kufa kwangu.

Mwenye dhamana ni Mungu tu, hizi ni sababu tu.

Kuhusu nyumba…

Kilichokuwa muhimu ukiandike kila unachokitaka kwenye wasia na muhimu zaidi sasa ni kumlilia Mungu kwa dua akuponye na kufaulu operesheni, na mimi nina hakika na hilo…kisha akatabasamu na kusema: “Usisahau, nataka uniletee zawadi kutoka Roma.”

Katarina alifuta machozi yake yaliyojaa bila kuyakusudia, kisha akatabasamu kwa maombi ya Adam…

Ndio…lililokuwa muhimu zaidi ni kunyenyekea kwa Mungu kwa dua, na zawadi gani utakayo Roma?

Ha ha ha, hakuna udi wa Kihindi au wa Kitaliano, wala sitokuletea zawadi za Kikatoliki kutoka Vatican.

Sitaki hili wala lile, nahitaji zawadi mbili, ya kwanza ni mkoba wa ngozi uliokuwa mzuri sana lakini rahisi sana, kama sio rahisi siutaki. Ya pili ninahitaji picha kubwa ya mchezaji Cannavaro, kwani yeye ni historia ya mpira wa miguu Italia.

Mkoba wa ngozi wa kifahari lakini rahisi sana, sidhani kama inawezekana….Ha ha ha ila kama tutampata Mutwi Rahman huko Italia.

Aliyemdharau Mutwi Rahman India, atamdharau Mutwi mwingine Italia.

Kwa mara ya kwanza nimegundua kuwa wewe ni mwana spoti!

Cannavaro alifuzu kwa tuzo la mchezaji bora katika Kombe la Dunia lililopita, na wahakiki na wakosoaji wa mpira wa miguu huko Italia wanaamini kuwa yeye ndie mrithi wa mfalme wa mpira wa miguu wa zamani wa Italia, Franco Baresi, kwa ujumla napenda kucheza michezo mbali mbali kuliko kushuhudia, hili ndilo ombi langu.

Hata ukitaka msalaba kutoka Vatican nitakuletea mimi, ikiwa Joji hatokuletea.

Kiasi gani mnaafikiana nami.

Asante mimi nataniana na rafiki yagu, je mwaniruhusu niondoke?

Wakati huo huo Tom aliingia ndani na kuona tabasamu na vicheko vingi.

Inaelekea kuna habari mpya Joji, nipe tumaini.

Hakuna jipya ila ni kuwa rafiki yangu anataka nimletee zawadi kutoka Roma; mkoba wa ngozi wa Kitaliano wa kifahari sana lakini ni rahisi sana, tulikuwa tunacheka kwa ajili hiyo.

Kutoka Roma?! Utakwenda Roma kufanya operesheni huko?!

Kwanza nakutambulisha kwa rafiki yangu Adam, na Adam na kutambulisha kwa daktari wangu na rafiki yangu Tom, operesheni yangu itakuwa leo na nitasafiri baada ya siku kumi kwenda Roma kutembea pamoja na mpenzi wangu Katarina na watoto wetu, na sijui nitamletea vipi mkoba?

Ni uzuri ulioje wa matarajio haya mema, kuna kilichobadilika kuhusu maudhui ya operesheni?

Hapana, lakini muono wangu wa maisha umebadilika kwa hisia ya matarajio mema aliyoniletea Katarina, na ambayo nimejifunza kutoka kwa Adam.

Ni kiasi gani tuna haja ya kujifunza matarajio mema, maradhi mengi ya nafsi suluhisho lake ni kuwa na hisia ya matarajio mema, lakini kuna ugumu katika kujifunza kwake.

Kaa na Adam, atakufundisha, ana hazina nyingi.

Kama ni hivyo nafurahishwa na mwanafunzi wake na kujifunza kutoka kwake.

Ukweli ni kuwa majibu mengi ambayo nayafanyia falsafa ninapokuwa nawe kwenye kikao nimeyapata ima kutoka kwake au kutoka kwa Katarina….Nakumbuka katika niliyokuambia: Tuchukulie mambo kwa wepesi wake bila uzito, hili nimelipata kutoka kwa Adam.

Vizuri sana, nukta hii haswa imebadilisha sehemu ya kufikiri kwangu na tabia yangu baada ya kuisikia kutoka kwako, tabia yangu au hata masomo yangu nimekuwa nikiyachukulia kwa ugumu wake.

Joji anajua kusifia ila ni kuwa mimi nakaa nae na kujifunza kutoka kwake, mimi ni mhudumu tu mgahawani, nae ni mwalimu wangu.

Katarina kwa tabasamu:

Kwa kuwa tumeanza kusifiana; hii ni juhudi ya Tom ambae alimaliza tatizo la maswali pekuzi yaliyokuwa yakimchanganya Joji.

Tom kwa mshangao:

Samahani ili kupata hakika, je operesheni ni leo?

Inaelekea hujaniamini, ndio….inaelekea bado unahitaji somo kuhusu matarajio mema, mambo yangu yote nimeshayapanga, nahitaji nipate muda wa nusu saa hivi pamoja na nafsi yangu, ili niandike baadhi ya karatasi, kwani uhai na mauti yapo katika mikono ya Mungu.

Operesheni ni saa ngapi?

Matayarisho yataanza saa kumi na moja jioni, na operesheni saa mbili usiku.

Adam aliangalia saa yake…

Nawaombeni ruhusa sasa hivi, inabidi niende mgahawani.

Nakushukuru sana Adam, wewe ni rafiki bora.

Subiri kidogo Adam, hii ni kadi yangu natamani kufahamiana nawe zaidi na kukaa pamoja.

Ni muhimu sana mkutane pamoja…..Adam inaelekea Tom amebadilika je sijakuambia hapo kabla….

Ni bahati kukutana nawe, samahani mimi sina kadi.

Kisha akatoa karatasi na kuandika jina lake na namba yake na kumpa Tom, kisha akaaga.

Pamoja na muda mfupi niliomfahamu Adam, nimemuona kuwa ni katika marafiki bora.

Ni mtu mzuri, nilipokuwa kwenye usingizi mzito na alipokuja Kakhi kunitembelea alionesha dharau kubwa kwake kwa sababu ni mhudumu, nae hakumwambia kitu, alichomwambia ni kuwa thamani yake ipo kwenye nafsi yake, inatoka ndani mwake, sio kutoka nje.

Ni muhimu nikutane nae na kufahamiana nae zaidi….kitu kizuri ni kuwa umekinai kuwa nimebadilika.

Simu ya Joji ililia, aliomba ruhusu kwa Tom na Katarina na kunyanyua, upande wa pili alikuwa mkuu wake wa kazi Kakhi….

Inaelekea hali yako ni njema sasa, nilikutembelea ukiwa katika usingizi mzito, vile vile alikuwepo mhudumu, vipi hali yako sasa?

Hali yangu nzuri, na mhudumu ni rafiki yangu, wala si ruhusu yeyote kusema yanayomchukiza.

Ha ha ha, nakupa habari nzuri…..menejimenti imeamua kukupongeza kwa kuweza kwako kusaini mikataba mitatu mikubwa kwa muda wa mwezi mmoja.

Nawashukuruni nyote, huenda ni kwa sababu nimetoa rushwa.

Achana na hiyo, lini utaanza kazi? Hukuomba likizo.

Sijui, leo nitafanyiwa operesheni, na baada ya hapo nitasafiri kwenda Roma kutembea, nitakaporudi nitaomba likizo, kisha nitaamua niendelee na kazi au la?

Inaelekea una hasira au umechoka, sijawahi kukuona ukizungumza hivi.

Kwa bahati mbaya nimevuka mipaka ya misimamo yangu, na nimekuwa chombo cha kutoa rushwa kwa Benjamin.

Kweli kabisa wewe una wasiwasi kwa sababu ya operesheni nitakupigia wakati mwingine, kwa heri.

Kwa heri.

Nini mpenzi wangu?

Kakhi, kinyume kabisa na Adam, hana adabu wala maadili!

Wengi mfano wake katika jamii yetu kwa sababu ya kuthamini fedha tu na kukana kwao Mungu na kuwa mbali na dini.

Tom akiongezea:

Kuwa mbali na Mungu ndio matatizo makubwa ya wanadamu ninavyodhani, na katika sababu kuu ni hofu na kupotea pamoja na majanga.

Angekuwa Katarina anasema hivi; nisingeona ajabu, lakini kulisema Tom hili ni jipya!!

Ha ha ha, je sijakuambia kuwa umekinaishwa kubadilika kwangu, na kwa upande mwingine tafiti zote zinathibitisha hivyo, lakini majanga ya kweli yapo kwa watu wa dini.

Unakusudia Upapa wa Katoliki.

Ninafahamu unacholenga, nimekuja tu kukujulia hali naomba mnipe ruhusa nitakuja kesho kukutembelea.

Asante Tom, nimefurahishwa na ziara yako.

Alipoondoka tu Tom…..Katarina alimgeukia Joji.

Kweli Tom amebadilika sana.

Ndio, dini hubadilisha kila kitu kwa mwanadamu.

Vizuri sana, inaelekea nawe Joji umebadilika vile vile.

Huenda ikawa hivyo!

Nitakwenda nyumbani kwa ajili ya watoto, kisha nitatenga muda kukuombea, na nitarejea saa kumi na moja.

Ni muhimu urudi nitakuwa nimemaliza kuyaandika katika karatasi ili nikukabidhi.

(3)

Joji alishughulishwa na alizama kuandika wasia wake, na kuhesabu mali anayomiliki, kwa muda wa saa moja alikuwa ameshamaliza. Kisha aliamua kuwaandikia marafiki zake wamuombee dua nakusali kwa ajili yake, na akawajulisha kuhusu operesheni atakayofanyiwa. Alipenda dua ziwe katika dini na madhehebu mbalimbali, huenda akajibiwa yule aliyekuwa katika haki. Alituma kwa rafiki zake, akikusudia haswa Habib Mkatoliki na Levi Myahudi –alitanabahi kuwa hana rafiki Muislamu, kisha akamkumbuka Mutwi Rahman na kumtumia na alipokumbuka India alimkumbuka Mbudha Jiyostana, lakini alijisemesha: Hawa ni wapagani, wao wanatengeneza Miungu yao, sidhani kama wananufaisha na kudhuru, nami nauchukia sana upagani…kisha akazima kompyuta yake.
Simu yake ililia, ilikuwa ni namba ngeni, akaitika.

Hallo habari.

Hallo Joji, tunataka kujua hali yako.

Ndio, nani mwenzangu.

Inaelekea umenisahau, mimi ni Levi kutoka Tel Aviv.

Ahaa, ok ok, nitamsahau vipi aliyenifanyia wema na kujifunza kutoka kwake? Nimekutamani sana Levi. Samahani sikuijua sauti yako, na sikutarajia kama utawasiliana nami.

Vipi habari za operesheni? Nina wasiwasi sana na hali yako…

Nashukuru hisia zako, nitafanyiwa operesheni leo, matarajio yangu ni kuwa itafaulu ila nimewatumia barua mniombee na kusali kwa ajili yangu.

Nitasali kwa ajili yako, lakini kwa bahati mbaya, nitasali Kiyahudi.

Kwa nini unasema bahati mbaya?!

Tokea uje huku nimekuwa nikisoma kuhusu madhehebu na dini mbali mbali pamoja na fikra mbali mbali; nami nitafute njia ya furaha, na bado ninaendelea kusubiri maelekezo yako kufikia furaha.

Nadhani umezidisha kidogo, mimi ndie ambae nimejifunza kutoka kwako, ni wewe uliyenifunza kuwa mkweli wa nafsi yangu….kabla sijasahau vipi rafiki yetu Habib?

Nipo nae hapa pembeni, anataka kuzungumza nawe.

Ha ha ha, mwambie ulinzi hadi kwenye simu. Habib ni mtu mzuri Levi jaribu kudumisha usuhuba wetu, rafiki ni mtu muhimu sana kwa mwanadamu.

Ha ha ha, kuna habari huenda Habib akakujulisha…La muhimu tutasali kwa ajili yako, nakutakia siha njema na nataraji utawasiliana nasi baada ya operesheni, huyu Habib ongea nae.

Hallo Joji, Mlinzi hapa, tupe habari nzuri, unaendeleaje na afya yako?

Leo nitafanyiwa operesheni, nitakuwa katika hali njema, vipi habari yako wewe, nimekutamani sana?

Sote tu wazima, na sisi tunakutamani sana, ziara yako ilikuwa ni ufunguzi wa mawasiliano na mijadala yetu.

Huku ni kutojikweza Dr.….Mimi najifunza kutoka kwako, na mazungumzo yako kuhusu madhehebu mbali mbali ya Kikristo bado yanavuma masikioni mwangu kwa mnasaba nitatembelea Roma na Vatican wiki inayofuata.

Vizuri sana, kamilisha safari yako ya furaha, umetuahidi kutupa habari zako.

Bila shaka, nitawapa habari ya safari yangu ya furaha; kwani hata Levi nimemuahidi hilo.

Nitakuambia habari inayofurahisha….huenda nikamuoa Levi.

Ooh, hongera, je ndoa itakuwa Kikatoliki au Kiyahudi?

Ha ha ha, ndoa haitofanyika ila baada ya miezi kadhaa bado kuna matatizo madogo madogo, huenda ikawa katika njia ipelekayo katika furaha vyo vyote iwavyo, Kiyahudi au Kikatoliki au Kiprotestanti.

Tunamuomba Mungu atusaidie kutuonesha njia ya kuelekea kwake.

Kwa amani ya Bwana, tunasubiri utupe tumaini ya afya yako na njia ya furaha, kwa heri.

Joji alikuwa mbali huku akifikiri…hakutanabahi na sauti ya nesi, ikimwambia:

Inabidi uondoke ukafanye baadhi ya vipimo.

Joji aliangalia saa yake ilikuwa ni saa kumi na moja kamili, Joji alimaliza baadhi ya vipimo na uchunguzi, na kurejea chumbani…alipoangalia saa yake ilionesha saa kumi na mbili unusu, Katarina alikuwa bado hajafika, alimpigia na akajibu kuwa yupo mlangoni hospitali anaingia, dakika chache akawa ameingia huku akiwa ni mwenye huzuni na kuomba samahani kulikuwa na tatizo katika gari lake, na hivyo kulazimika kupanda basi na ndicho kilichomchelewesha.

Nilipatwa na wasiwasi nilipoona umechelewa.

Nami nilihofia nisije kuchelewa zaidi ndio maana nikaliweka gari pembeni na kupanda basi.

Chukuwa hii bahasha, ina makaratasi yote na nyaraka mbali mbali ambazo utazihitajia kukitokea lolote baya kwangu.

Utakuwa katika hali nzuri apendapo Mungu.

Kuna kitu ambacho sijakiandika.

Kitu gani?

Nataka ukamilishe utafiti wangu kuhusu njia ya furaha kwa ajili yako na watoto.

Utakamilisha njia hiyo mwenyewe, na utafanikiwa muradi wako, Mungu hatokuacha kamwe, wewe ni mwenye tabia njema na maadili.

Futa machozi yako….kisha nipe ahadi Katarina.

Nina kuahidi kuwa nitakamilisha utafiki wa njia ya furaha pamoja nawe Mungu akipenda na utafiti wa mwanzo utakuwa pindi tukiwa katika safari yetu Roma.

Nakupenda Katarina.

Kisha akamsogelea na kumkumbatia…na Katarina akaangua kilio.

Nami nakupenda Joji.

Kuwa mwenye matarajio mema kama ilivyo ada yako, je umeshaweka nafasi ya hoteli Roma?

Ndio.

Kwa mara nyingine tena nesi aliingia chumbani na kumchukua Joji akamalize uchunguzi…Joji alimshika Katarina mkononi kwa nguvu na kumtaka arudi nyumbani, na kumuombea….

Nenda nyumbani mpenzi wangu baada ya muda watanichukua kwenda kwenye nusu kaputi na operesheni itachukua masaa matatu…huna haja ya kukaa, nitakuwa katika hali nzuri, usijali…

Usiseme hivi, mimi nakupenda Joji tutasafiri pamoja kwenda Roma, na tutapata njia ya furaha.

Mama unaweza kuondoka sasa, tutawasiliana nawe baada ya operesheni, tunayo namba yako.

Bwana akulinde Joji, na akubarikie katika umri wako na maisha yako.

Joji alipelekwa kwenye chumba cha operesheni na moyo wake ukitiririka hofu ya Katarina na wanawe, hakuiogopea nafsi yake kamwe, alikuwa akifikiria dunia itakuaje lau kila mmoja hamu yake itakuwa ni kwa ajili ya nafsi yake tu? Ni jambo lisilo vumilika, kubeba huzuni za watu na maumivu yao hupunguza katika nafsi ya mtu uwezekano wa maumivu. Vivyo hivyo maisha, atakayeishi kuhudumia watu na kuwafurahisha atakuwa na furaha na atakayeishi kwa ajili ya nafsi yake atapotea njia…Daktari alikata fikra zake zilizokuwa zinatiririka akimwambia:

Nakutaka uwe katika hali ya utulivu kabisa, uchunguzi wa mwanzo ni mzuri sana, halitokuwa ila kheri tupu.

(4)

Operesheni ilimalizika usiku wa manane, ilichukua muda wa masaa manne, Katarina alikuwa akipiga simu hospitalini kila baada ya saa moja, wala hakutulia ila baada ya daktari kumpigia simu alipotoka chumba cha operesheni, na kumjulisha kuwa mambo yamekwenda vizuri na ya kuwa matokeo ya operesheni yatakuwa tayari baada ya masaa kumi na mbili, naye Joji hatozindukana ila baada ya muda huo takriban….

Poa bibiye, na wajulishe wengine wanaopiga simu, kwani mawasiliano hayakatiki hospitalini.

Ni nani wanaopiga simu?

Ni Adam na Tom…kama unawajua tafadhali wajulishe.

Vizuri, nitawajulisha wasali kwa ajili yake.

Ilikuwa inakaribia saa kumi na mbili siku inayofuata…. Joji alianza kuzinduka, na kutingisha mkono wake katika hali isiyokuwa ya kawaida, na kutoa maneno yasiyofahamika Katarina, Adam na Tom waliokuwa wamekaa wamemzunguka hawakujua analosema….ila maneno machache tu: Njia ya furaha, kwa nini tumeumbwa, uhai…kifo.
Daktari alifika kuangalia hali ya Joji, Katarina akasimama upesi. Daktari akatabasamu.

Najua hofu yako bibiye….nakupa habari nzuri ya kuwa uchunguzi wote ulikuwa mzuri, tunatarajia kuzinduka baada ya muda mfupi.

Lakini daktari, yeye anazungumza maneno yasiyofahamika?

Msiogope! Bado hajaondokana na nusu kaputi na akaweza kuzungumza kwa uwazi, hiyo itakuwa ni alama ya kufanikiwa operesheni. Kesho tutamuondoshea mashine, akiweza kutingishika kisha kusimama, hii itakuwa ni dalili kuwa operesheni imefanikiwa kwa asilimia mia moja. Akizindukana tu, tutampa vitulizo vya maumivu kila baada ya masaa matatu, na baada ya hapo mtamuona akiwa mzima kabisa. Kuweni na matumaini.

Asante sana, Mungu atamuhifadhi.

Kwa mnasaba ni kuwa akiwa katika nusu kaputi kila mara alikuwa akirejea maneno “Njia ya furaha”, ni nini hiyo njia ya furaha aliyokuwa akisema?

Ni njia anayoifanyia utafiti, imemshughulisha sana, anataka kuigundua.

Ni mmoja katika watu wachache waliofika katika hospitali hii akiwa mwenye furaha, kwa nini basi anatafuta furaha?

Alianza kuwa na furaha pindi alipoanza utafiti wake huu.

Atapata kwa uwezo wa Mungu. Haya kwa herini.

Alipotoka tu daktari, Tom alimgeukia Joji aliyelala chini ya uangalizi wa mashine na akanong’oneza kwa masikitiko.

Kabisa utapata njia ya furaha Joji, nami nitakuwa nawe, nilipita njia nyingi, njia zenye tabu, ukanaji wa Mungu na sikuambulia chochote isipokuwa huzuni na ghamu tu. Hata hivyo hadi wakati huu sijakinaishwa na dini yoyote, pamoja na kukinaishwa kuwa Mungu mwenye huruma ndie aliyetuumba na ndie mwenye uwezo wa kutuongoza.

Mimi nina hakika ewe Tom utaipata.

Nitaipataje Adam?

Nasema ulichokisema kuwa Mungu Mwenye huruma hamuweki mbali anayetaka kuwa nae karibu, na hivyo basi sote; mimi, wewe na Joji tutapata tunachokitafuta.

Nawe unatafuta njia hiyo?

Huenda hivyo!!!

Joji alianza kufungua macho kwa tabu. Katarina alitanabahi na akasogea karibu nae.

Mpenzi wangu Joji je unanisikia?

Ndio.

Namshukuru Mungu kwa salama yako, tulikuwa tuna wasiwasi sana nawe, Adam na Tom hawa hapa wamekuja kukujulia hali.

Asante.

Tunakutakia kila la kheri upone haraka.

Nami nakutakia kila la kheri upone haraka, daktari ametupa habari nzuri kuwa operesheni imefanikiwa.

Je unataka chochote mpenzi wangu?

Hapana.

Naona tumuache, tusimtie uzito, ataamka pole pole.

Kweli kabisa, nashauri mimi na Adam tuondoke na ubaki wewe pembeni yake.

Nakushukuruni sana, atawapigia mwenyewe leo awajulishe hali yake mwenyewe.

Je Adam unayo gari au ungependa nikupeleke?

Hapana, sina gari, wala sipendi kukutaabisha, nitachukua basi.

Panda nami, nataka kuzungumza nawe kidogo, kwa heri Katarina.

Kwa heri.

Baada ya kuondoka kwa Adam na Tom kwa nusu saa….Joji alifunua macho yake tena, wakati Katarina akiwa mbali na kuwaza….

Katarina.

Joji mpenzi wangu vipi hali yako?

Nzuri…Kama kwamba nilimuona Tom na Adam?

Wameondoka sasa hivi, baada ya kujua hali yako, walikuwepo hapa tokea mapema asubuhi sana…..Vipi mpenzi hali yako?

Saa ngapi?.....Nasikia maumivu kichwani.

Inakaribia moja usiku, usijipe tabu nitamwita daktari sasa hivi.

Daktari alikuja upesi alipoitwa na nesi.

Inaelekea hali yako ni nzuri Joji.

Kuna maumivu makali kichwani.

Hamna neno, utapewa kitulizo cha maumivu, na yote yataondoka, hii ni hali ya kawaida, kwani sehemu ya kichwa kilifunguliwa, hali hii ni nzuri inatupa matumaini.

Ameanza kuzungumza vizuri, pamoja na uzito.

Hizi ni dalili za kufanikiwa operesheni, tumaini, na Joji vile vile atumaini.

Asante.

Daktari alimpiga Joji sindano ya kutuliza maumivu…kisha akamgeukia Katarina, na akamnasihi aondoke, kwani Joji atalala muda wa masaa mawili baada ya sindano kwa uchache.

Bali nitasubiri pembeni yake.

Akisha amka atapigwa sindano nyingine kwa masaa mawili au zaidi, maamuzi ni yako.

Mpenzi wangu nenda.

Nitasali kwa ajili yako siku nzima.

Saa moja unusu asubuhi Joji alikwisha zinduka, alizungumza na nesi kwa lugha inayofahamika iliyo wazi kabisa, pamoja na kuwa alikuwa anaendelea kulishwa kwa kutumia mashine ya kulishia, na muda huo ilikuwa bado hajapewa chakula…
Katarina alimpigia simu na kuzungumza nae na kumtuliza, na akamtaka awapitie Adam na Tom, nae akawapitia kisha Joji akawasiliana na Habib na Levi…baada ya hapo akajisalimisha katika fikra zake kuhusu njia ya furaha na safari yake ya Roma.