MASWALI MENGI YENYE UTATA

MASWALI MENGI YENYE UTATA

MASWALI MENGI YENYE UTATA

(1)

Katarina alimgeukia Joji mara tu baada ya kuisha filamu ambayo walikuwa wanaangalia pamoja. Alifanya hivyo ili amwondoe katika ukimya ambao alikuwemo pengine akili zake zilikuwa zimekwenda mbali.

Joji ..Joji…hivi hutaki kuondokana na matatizo uliyokuwa nayo?

Unasema niniuna maana gani? Bila shaka nataka niondokane na matatizo yangu.

Jirani yetu mpya aliniambia kuhusu tabibu nafsi mashuhuri anaitwa Tom Erickson.? Aliniambia kuwa yeye alipata kutibiwa naye.

Joji aligeuka katika kiti chake na akamwangalia mkewe na usoni alikuwa tayari kuna ndita ikiwa ni ishara ya kuwa hakuwa na utulivu tena wa nafsi. Kisha akasema kwa dharau…

Vizuri sana, wataka niende kwa huyo tabibu kisha niseme –nieleweshe maana nasahau kwa nini niliumbwa na kwa nini naishi?

Hapana! Bali mwulize akuambie njia gani utumie kufahamu kwa nini uliumbwa na kwa nini unaishi?

Ili nijue jawabu!!!

Ndiyo.

Joji alilaza kichwa chake kwa nyuma hakukaa hivyo sana bali akaingiwa na wasiwasi na shida. Katarina akaliona hilo na akatambua kuwa Joji hapo alipo hana mawasiliano tena bali kaingiwa na wasi wasi na hofu tena. Basi akamwita kwa sauti kubwa.

Joji!

Naam, naamnilikuwa nataka kukuuliza huyo dokta Tom ni Mprotestanti? Au hamasa zako ni kwa sababu zingine?!

Joji mpenzi! Hamasa zangu ni kutaka mimi nawe tuishi kwa furaha. Pengine una chukizwa na vile ninavyoikimbia nafsi yangu. Lakini hilo ni bora kuliko hivyo unavyoishi kwa wasiwasi na mashaka.

Vizuri nilikwisha fanya uamuzi kuwa nitafute njia ya kuelekea kwenye furaha. Sintokimbia na kujificha katika ndoto kuanzia leo, badala yake nitatafuta jawabu hilo…kisha Joji alitabasamu na akaongeza kusema: Lakini sitoifuata njia hiyo ndani kwa padri wa Kikatoliki. Jambo la kwanza nitamtafuta huyo daktari kwanza.

Tutauliza habari zake na namwomba Mungu ajalie katika mikono ya daktari huyo tiba.

Hahaha! Maana yake mimi ni mgonjwa ambaye anahitajia tiba –mimi siyo mwana falsafa anayetafuta majibu ya maswali!

Tiba ndio njia ya kufikia majibu siyo kuwa wewe ni mgonjwa – kisha Katarina alimkonyeza na akajitupa kifuani kwake na akasema:Tumeelewana mpenzi?

Tumeelewana!

(2)

Joji alikuwa makini sana kutaka kujua habari za dokta Tom kabla hajafanya mpango wa kuenda kumzuru. Alifungua mtandao wake wa – facebook akaona mikutano ambayo alipata kuhudhuria dokta Tom. Akaona aina na jinsi ya mihadhara aliyopata kusikiliza na ile aliyopata kutoa. Kisha akasoma yale waliyoandika wagonjwa wake kuhusu yeye, akapata picha ya alivyo dokta Tom, ni daktari makini wa magonjwa ya nafsi, mwerevu, mwenye taaluma pana, mpenzi wa falsafa, alikuwa ni mtaalamu aliyechanganya taaluma za kisasa za tiba na masomo mbali mbali ya falsafa.
Joji alifuatilia rai za wagonjwa wa Dk Tom na maelezo yao, kwa njia hiyo aliona kuwa tabia za Dk Tom na elimu yake vilikuwa haviendi sawa sawa, hususan na wagonjwa wake wa kike. Na pia akaona kuwa huyo si Mkatoliki kama alivyo kuwa anadhania, bali huyo bwana ni mpagani, haamini dini yoyote.
Joji alikuwa anachelewesha kupanga siku ya kwenda kwa dokta Tom, aliakhirisha mara nyingi, hakuwa na haraka na hakupenda kwenda kwa dokta mwenye tabia yenye kutatanisha. Lakini alimwahidi Katarina kuwa atakwenda na akaendelea kutoa sifa zake mganga huyo kwa mkewe. Basi siku moja ghafla mkewe akamshtukiza na kumwambia amepanga waende siku hiyo kwa daktari saa kumi jioni na watakwenda pamoja. Kwa shingo upande alikubali, lakini hakuwa na raha kwa kukutana na daktari huyu! Alikuwa akijisemeza: Uzoefu mpya lakini utakaofeli, si tatizo halitonidhuri lakini utafunga mdomo wa Katarina.
Joji na Katarina wakaenda katika kliniki ya dokta Tom siku hiyo, ilikuwa ni kliniki tulivu kabisa, samani zake ni nzuri za kuvutia, rangi zake zimeshikana vizuri na zinafurahisha kuziangalia. Mahali pa makaribisho walikuta mtu mwenye sura yenye mikunjo mikunjo, amekaa ametulia mezani. Joji akamueleza kuwa walikuwa wamepangiwa kumwona dokta Tom saa hiyo, na akajibu kwa utaratibu kabisa:

Naitwa Baraad, sijapata kukuona kabla ya leo. Nadhani daktari ana kazi sasa hivi.

Joji alimgeukia Katarina na akamuuliza?

Je, hukuweka ahadi ya kukutana na daktari leo?

Bila shaka nilikuja siku tatu zilizopita na kuweka ahadi!

Baraad akajibu kwa utani,

naam …naam nilisahau nisamehe, kweli uliweka ahadi, tafadhali ingieni anawasubiri.

Joji na Katarina wakaingia ofisini kwa daktari huku Joji akishangazwa na kuchukizwa na tabia ya Baraad. Daktari aliwapokea vizuri, kisha akaomba akae na kila mmoja wao peke yao.

Joji akasema:

Lakini mimi tu ndiyo niliyepanga kukuona.

Na Katarina mkeo, na watu wengine ambao wako karibu yako, hao watanisaidia sana katika kufahamu hali yako. Napenda nikae naye kwanza kabla yako kwa muda, kisha nikae nawe.

Joji alitoka akaenda chumba cha makaribisho akaketi kwenye kiti kimoja akiwa kimya tena kwa tabu. Baraad akaanza kumsemesha:

Tom yuko na Katarina!

Wewe nani kakwambia jina lake?

Ah! bwana! siyo huyo mama aliyekuja hapa siku tatu zilizopita…kisha akatabasamu kiutani. Tom anakaa nayewawili tu peke yao, kwa kweli dokta Tom ni mwenye bahati sana. Mwanaume anayependeza anakaa na mwanamke mwenye mvuto wa nchi za Mashariki!

Joji akawa hana raha akatafuta jarida limshughulishe na kumweka mbali na Baraad ili kuficha hasira zake. Kisha Joji akakumbuka sifa mbovu za Tom na mahusiano yake na wagonjwa wake wa kike. Ilikuwa kidogo avunje ukimya, lakini akajikaza basi akaamua kunyamaza. Baada ya kimya kama dakika kumi hivi akatoka Katarina na huku akicheka na kumwita mumewe:

Mpenzi! daktari anakusubiri. Mimi nakwenda Kanisani kuna jambo nimepanga kulifanya huko.

Joji aliingia kwa daktari na ule uchangamfu wake ukapotea. Akapokelewa vizuri lakini katika uso mkavu wa daktari na akamwambia:

Kwa nini unataka kujua nani aliye kuumba? Na kwa nini unaishi? Na unaelekea wapi?

Kwa sababu nataka niwe na mpango wa maisha na roho yangu itulie nikijua maana ya maisha na uhai wangu.

Mh mh! Hapa naona niko na mtu mwenye elimu kubwa msomi mzuri! Kwanini hutumii njia za wanafalsafa katika kufikiri na kuwaza?

Sikuelewi, una maana gani?

Vipi hufahamu ewe mwanafalsafa? Tunapotumia kujibu mambo kwa njia ya falsafa mambo yote yanajipanga kwa mpangilio wa maswali moja baada ya jingine na kuleta majibu yake vivyo hivyo.

Alinyamaza kidogo kisha akaendelea kusema:

Ili kuweza kujibu maswali yako nitakuuliza maswali mengine, kwa mfano: ni wapi tunaweza kupata majibu ya maswali haya? Badala ya kutafuta na kuyaingia majibu moja kwa moja, tuangalie tunaweza kupata wapi? Ni yepi vigezo vya usahihi wake? Je huoni ya kuwa njia hii ndio ya mantiki ya kifalsafa nzuri zaidi?

Huenda ikawa ni hivyo!

Njia hii hutumika katika kuleta majibu ya maswali yako kutoka kwako mwenyewe –rohoni mwako! Kisha akatabasamu na kusema: Bila shaka hii ni njia bora kuliko njia ya Wakatoliki ambayo ni kukubali kila kitu bila ubishi au kutumia akili! Tukutane tena juma lijalo na ujitahidi uniletee majibu juu ya maswali mawili: la kwanza ni wapi tunaweza kupata majibu? Nini dhamana ya usahihi wake? Je tumekubaliana?

Licha ya ubaya uliosema juu ya Ukatoliki ila ni jambo la mantiki na linaingia akilini, sawa tumeafikiana.

Joji alitoka hapo kwa tabibu na mara jicho lake likamwona Baraad ambaye alimuwahi kwa tabasamu lake zito la kijanja janja.

Natumai kikao chenu kilikwenda vizuri, salamu zangu kwa Katarina!

(3)

Maswali ya Tom na njia zake za mazungumzo zilimwathiri sana Joji. Akawa anaendesha gari lake na huku anajizungumzisha. Mimi nilikuwa na maswali lakini Tom kaniongezea maswali kichwani mwangu!
Akaelekea kwenye mgahawa wa karibu ili akapate kikombe cha kahawa. Alifika mhudumu na akaiweka kahawa hapo mezani, lakini yeye hakuhisi chochote. Mhudumu alijaribu kumtanabahisha lakini Joji alikuwa amezama ndani ya mawazo mazito. Aliondoka mhudumu. Baada ya muda Joji alizindukana kuiona kahawa yenye vuguvugu hapo mezani. Alimuita mhudumu aje amlipe:

Hivi unaamini kuwa sikuhisi pale ulipo kuja na kahawa, Ah! Wajuwa wakati mwingine akili zetu zinashughulishwa na maswali yetu ya ndani hata nafsi zetu na mtu anajisahau!

Mtu kuwa na maswali mengi kichwani ni dalili ya kuwa ana akili na mtu aliye makini, lakini hali hiyo ikizidi, basi huo ni mkorogano wa mambo ya ndani yake, na mgongano kuhusu lipi lenye kukinaisha katika fikra za mtu.

Joji alishangazwa na maneno ya mhudumu na akaendeleza mazungumzo naye:

Ni nini chanzo cha mkorogano huu – nipe rai yako!

Vyanzo ni vingi. Vilivyo vikubwa ni kuwa mtu hakuangalia vitu vya msingi na kuviangalia kwa dhati yake na haswa vile ambavyo anaishi kwa ajili yake kama vile: Kwani tumeumbwa? Kwa nini tunaishi? Na wapi tunaelekea? Tatizo hili huwa limefichikana kwenye itikadi, utaratibu na wepesi wa maisha utatupa kuzama katika majibu ya maswali yale.

Joji alifungua macho yake kwa mshangao:

Vipi mtu afikie majibu ya maswali hayo kwa wepesi?

Watu wengi huyakimbia majibu ya maswali hayo kwa kuendekeza michezo na ulevi au kufanya uasherati na mambo mengine ya namna hiyo. Na kujiuliza kuhusu mambo hayo ni katika dalili nzuri ya mtu kuwa na utambuzi wa mambo, lakini…

Mhudumu aliitwa na mteja mwingine na akakata mazungumzo yao haya mafupi. Aliomba radhi kwa Joji na akachukua malipo yake ya kahawa na kuondoka.
Joji alitoka hapo akawa anazunguka na gari lakehajui anakwenda wapi, lakini hakuweza kusahau maneno ya mhudumu. Maneno hayo yalimpata akilini na kukamata hisia zake. Alikuwa anatamani yule mhudumu angelifikisha mwisho kauli yake. Na lau hilo lingemfanya alipie tena bei ya kahawa mara kumi hivi! Alikuwa anashangaa kuwa kwake na furaha sana alipokuwa anazungumza na mhudumu huyo licha ya kuwa ni mtu wa chini sana, kama vile ilivyo kazi yake ni ndogo, sura na umbile lake linaonekana kuwa ana asili ya Ugiriki basi kama sivyo ana asili ya Kilatini.
Baada ya kama saa hivi kupita, Joji alitanabahi kuwa bado hajatoka kule alipokuwa, aliamua kurudi katika mkahawa ule kwa mara nyingine, alifika akakaa mezani na akaagiza kahawa kama mwanzo. Akaja mhudumu mwingine akamwuliza kuhusu alipo yule mhudumu wa mwanzo.

Ni yupi unayemkusudia Bwana?

Nilikuwepo hapa kabla ya nusu saa hivi na alinipokea mhudumu mwingine.

Pengine huyo ni Katu au Adam hao zamu yao imekwisha kama saa moja hivi, na sasa ni zamu yetu.

Joji akanywa kahawa haraka haraka na wakati akiondoka alimuuliza yule mhudumu:

Lini watauwa kazini Katu au Adamu?

Kesho saa tatu asubuhi watakuwepo mpaka saa kumi na moja au kumi na mbili jioni.

Ahsante sana!

(4)

Joji alirejea nyumbani kwake na watoto wake wakampokea. Akawauliza mama yao yuko wapi. Maiko akamwambia kuwa bado yuko kanisani na pengine atachelewa kidogo hadi usiku.
Joji akaketi barazani akimsubiri Katarina arudi kutoka kanisani. Hakurudi mpaka saa nne usiku, yuko hoi anajisukuma, ananuka pombe, pamoja na kuwa alikuwa akitambua kilichokuwa pambizoni mwake. Pindi tu alipomwona Joji akamuuliza:

Vipi habari kuhusu daktari?

Ah! Ni daktari wa ajabu, pamoja ya kuwa kuna mambo ambayo yuko makini nayo. Joji akamgeukia Katarina na kumuuliza: Alikuwa anataka nini mlipo bakia pamoja?

Sijui mpenzi, alikuwa ananikaribisha tu, kisha akajitambulisha yeye na uwezo wake, kisha akauliza kazi niifanyayo na maisha yangu kwa ujumla. Ni mwepesi kuelewana naye na ni mchangamfu sana.

Na bila shaka ni mwenye umbile zuri! Je, hakukuuliza habari zangu hata kidogo?

Aliniuliza pale nilipotaka kuondoka. Nikamweleza kuwa unapatwa na woga na unakuwa na fikra nyingi hasa juu ya maisha.

Hilo tu?!

Hilo tu! Muda mwingi alikuwa anazungumza habari zake na kuniuliza mambo yangu, kiasi gani alivyo na heshima zake.

Mh mh! Meneno ya ajabu juu yake. Unamsema vizuri licha ya kuwa ni mpagani hana dini na anapiga vita dini zote na anaona kuwa mtu kuwa na dini ni maradhi, kwa kweli ni mpuuzi!

Joji! Alikuwa ni mtu mwema kwangu! Hakuzungumza nami kabisa kuhusu mambo ya dini, hata baada ya kujua kuwa mimi ni mwalimu wa dini. Hata hivyo shida yako kwake si adabu yake wala dini yake!

Ulikuwa na nani mnakesha jioni hii na mkinywa?

Huna haja ya kuniusia, na ni haki yangu kutokujibu. Hata hivyo tulikuwa tuna hafla kanisani ya kumbariki padri.

Mara nyingi Joji hupata shida pale Katarina anapokesha kanisani na kuchelewa kurudi nyumbani usiku, na hasa anapo kunywa maana hilo linapingana na dini yake ambayo huyu bibi hutumia muda mwingi akiitumikia. Hata hivyo Joji alihisi kuwa alimkosea Katarina kidogo, Joji akabadilisha mwelekeo wa mazungumzo kwa kutania:

Nilikuwa na maswali kadhaa, basi yule bwana akaniongezea tena maswali tele juu ya maswali yangu na kuzidi kunivuruga tu.

Vipi?

Badala ya kutoa majibu kwa maswali yangu, akaniuliza maswali mengine na akataka nimpelekee majibu.

Maswali mengine?

Naam! Nitapata wapi majibu ya maswali hayo, na je kipi kitahakikisha usahihi wa majibu hayo.

Pamoja na kuwa ni maswali ya ajabu huenda akawa ni mwenye haki kufanya hivyo!

Achana na hilo! Leo nimekutana na mtu mwingine wa ajabu. Kanichezea akili yangu sana. Kasema maneno yanayonigusa bila kukusudia. Kasema habari zile zile nilizofuata kwa yule daktari.

Habari zile zile?!

Eh! hiyo ni ajabu ya mambo!

Kasema nini huyo mtu?

Sielewi kwa uwazi wake, maana hakumaliza kusema maneno yake, ingawaje anaonekana kuwa ni mtu mwenye dini tofauti kabisa na alivyo Tom. Alikuwa akizungumzia wepesi wa kujibu maswali, na kuzama katika hili, maana ya maisha na furaha, kisha Joji akamkazia macho mke wake: kazungumza pia kuhusu watu wengi wanavyoyakimbia majibu kwa kuzama katika kunywa pombe na kukesha na mfano wa hayo!

Kwa kuwa ni mtu wa dini, basi maneno yake yalikuwa mazuri, kidogo alikuwa mkali juu ya watu kukimbia ukweli wa majibu!. Katarina alitabasamu na kusema: Pengine alikuwa Mkatoliki! Mpenzi wangu unaonesha umechoka na huwezi kuwa makini na unachozungumza!

Labda hivyo lakini alinigusa sana kwa hali zote. Tulale sasa kesho nina kazi nyingi.

Wakaondoka hapo barazani kwenda chumbani kulala kabla ya usingizi simu ya Katarina ikaita, aliangalia akiwa ni mwenye kubabaika, kisha akamjibu aliyempigia kwa maneno ya haraka haraka kisha akabakia kimya akisikiliza kwa muda mrefu kisha akakata simu.

Ahadi yetu ni Jumatano saa mbili usiku, tutakesha pamoja kanisani.

Nani huyo aliyepiga simu?

Mtu ambaye anataka kujifunza Ukatoliki.

Anajifunza katika mkesha!

Mkesha kanisani na si katika jumba la dansi au unataka akajifunze dini makaburini. Hebu tulale acha mambo yako.

(5)

Kulipokucha Joji aliamka kabla ya Katarina na jambo la kwanza kichwani mwake ni habari za yule mhudumu ambae hajui siri ya kuvutika nae, aliazimia kwenda mkahawani kukutana nae tena. Mara akakumbuka simu iliyokuja kwa mkewe jana usiku. Aliifungua simu ya Katarina akanakili ile namba ya yule aliyepiga usiku kisha akairejesha simu mahali pale pake.
Joji aliondoka akaenda kazini mapema, alifanya hivyo kwa kuwa jana aliomba rukhsa atoke mapema na kazi zikarundikana mezani kwake wakati alipo kwenda kwa Dk Tom. Alipoingia ofisini kwake na kuanza kufanya kazi zake mara alipigiwa simu ya mezani. Huyo alikuwa ni Kakhi mkuu wake wa kazi.

Habari za asubuhi!

Njema bwana!

Vipi ziara yako kwa dokta jana ilikuwaje?

Hamna tabu! Ilikuwa salama, bado ndiyo mwanzo mambo yatabainika huko usoni.

Vizuri! lakini unapoteza muda wako na fedha kwa kufikiria juu ya mambo haya ambayo ni kazi bure tu. Kwa upande wangu kama ungeniuliza ni nani atakayenilipa zaidi nitamfanya kuwa ni Mungu wangu kisha akacheka kicheko kikubwa, na akasema: hebu njoo kwangu kuna kazi iliyotokea jana.

Sawa! nakuja baada ya saa hivi ikiwezekana.

Vema! njoo baada ya saa moja.

Joji alipiga namba ile iliyotumika jana usiku ila hakutumia simu yake, alisikia sauti ya Tom upande wa pili. Joji hakukosea sauti aliyoisikia, alimsikia akisema: Hallo haloo nani mwenzangu? Je, unanisikia? Joji alikata simu mara moja, ghadhabu ilimmiliki, kwanini Katarina hakumwambia kuwa aliyempigia simu alikuwa Tom? Na kwa nini alibabaika? Kwa nini…? Je, ndivyo yalivyo maisha ni siri ndani ya siri na maswali mengi?
Joji akarejea kufanya kazi zake ili amalize kazi zake kwa haraka. Na baada ya saa moja kamili alifika ofisini kwa Kakhi, Khaki alisimama na kumkaribisha.

Rafiki yangu! Vipi dokta kakutibu wasiwasi wako?

Bwana mie sina wasiwasi wala mimi siumwi! Nilikwenda kwa dokta ili anipe majibu ya maswali yangu.

Inaonekana kuwa maudhui hii ni nyeti sana kwako, nilikuwa na kudhihaki tu. Unajua rai yangu kuhusu hilo, achana na hayo kwa sasa, la muhimu napenda ujali namna ya kujiongezea mali zako na ufurahie maisha yako na raha zake.Nimekuita tukutane mimi nawe kwa sababu shirika la ugavi na teknolojia huko India limetutumia muwafaka wa sharti zetu, nasi kwa sasa tuna haja ya kuchukua watu kutoka kwao, kama ilivyo tuna haja ya kukuza uhusiano wetu na shirika la ugavi wa programu huko India. Ni lazima mtu mmoja aende

India katika kipindi cha majuma mawili kuanzia sasa! Je uko tayari kusafiri?

Haraka hivyo?

Kwa bahati mbaya ndiyo. Mimi kwa bahati mbaya siwezi kwenda kwa sababu kutakuwa na kikao cha bodi baada ya majuma mawili.

Nitaangalia vipi itakuwa nafasi yangu, na nitakueleza kwa siku mbili hizi kama ninaweza kwenda au vipi. Ningelipenda ungelinipatia nakala ya mkataba na makubaliano ndani ya mfumo wa mtandao; ili niuthibitishe na kuufanyia utafiti ili mambo yawe wazi kwangu.

Hivyo basi miadi yetu ni juma lijalo! Ni vizuri ukajitayarisha na safari..kisha tabasamu na achana na huyo tabibu, nina jambo nitakalokushtukizia wiki ijayo.

Joji alitoka nakwenda ofisini kwake. Aliangalia ile mikataba na nyaraka za maelewano ya mwanzo ambavyo Kakhi alikuwa kamtumia tayari kupitia mtandao wa ndani wa shirika. Joji aliitamania sana hiyo safari, lakini alikuwa ameshughulishwa na mambo matatu: Mhudumu, daktari pamoja na Katarina!
Toka asubuhi ya leo alikuwa ameazimia kwenda kumwona mhudumu. Ama tabibu miadi yake naye ni kabla ya safari, na inawezekana kabisa kuomba miadi nyingine siyo ile iliyopangwa, Lakini Katarina!? Hivi inaingia akilini kuwa mkewe ambaye ni mchaMungu anafanya khiyana ndani ya ndoa yao kwa Tom mpagani? Vipi hilo. Hapana mbona haliwezekani!!
Muda wa kazi ulipomalizika Joji alielekea kwenye mkahawa wa jana ili akaonane na mhudumu wake wa jana. Alipofika na kumwona basi nafsi yake ikatua akashangaa kuhusu hilo, kisha akaketi mezani na yule mhudumu akaja kutoa huduma:

Naam! nikusaidie nini kaka!

Kahawa! Samahani! hivi wewe waitwa Katu au Adam?

Naitwa Adam kaka!

Mhudumu alindoka kwenda kuleta kahawa na mara aliporudi Joji akaanza kusema:

Hivi waweza kupata muda tukakaa na kuongea mimi na wewe?

Samahani kaka sitoweza, natamani kukuhudumia, lakini nina majukumu mengi.

Vipi Je, ninaweza kukusindikiza unapo maliza kazi zako.

Ah! huo ni ukarimu wako kwangu hilo nalikubali! kwa uchache leo sitalazimika kupanda mabasi... muda wangu wa kazi una kwisha baada ya nusu saa.

Sawa basi nitajivuta kidogo kidogo katika kunywa kahawa ili niisubirie iishe, nitafurahi kukusindikiza.

Ahsante sana kwa hilo, kwa idhini yako.

Joji akawa anakunywa kahawa yake pole pole, huku akikumbuka yale maneno ya Adam yaliyomtingisha, akawa anajiuliza: mhudumu huyu ananishangaza sana, amewezaje kunielewesha kwa haraka wakati hanifahamu? Alijuaje kuwa nina matatizo ya kifikra kuhusu kadhia nzito kama hizi? Nina hamu ya kujua majibu yake…kwa undani zaidi na kwa wepesi..ehe falsafa iliyoje!
Adam alitokea na kukatisha mawazo ya Joji na akamwambia huku akitabasamu na akiwa amevaa nguo za kawaida baada ya zile za kazi akasema:

Mimi niko tayari! Je tuondoke?

Nami pia, Je wataka kwenda nyumbani kwako au tukapate kahawa hapa hapa au twende tukapate chakula cha jioni katika hoteli ya karibu?

Kama umenipa uchaguzi katika hayo basi nachagua la tatu.

Kuna hoteli ya furaha hapa karibu nafikiri itatufaa.

Hiyo inafaa kabisa! Jina lake lina mvuto yaani furaha jina zuri sana na watu wengi hawaipati hasa katika zama zetu hizi kuna tabu tupu na mashaka.

Maneno ya Adamu yaligonga kifuani kwa Joji aliona kama vile alikuwa amelengwa yeye lakini aliamua kumezea asijibu kitu.

(6)

Joji na Adam waliingia hoteli ya furaha na wakaikuta kuwa inafurahisha kweli; kwa rangi zake na mapambo yake vilikuwa vinapendeza. Mipangilio yake ilikuwa ina mweka mtu katika furaha na raha.
Walikaa mezani na akawajia mhudumu akiwa na orodha ya vyakula (menu) na Joji akamwambia Adam;

Tafadhali, chagua chochote.

Nakula samaki aliyekaangwa na mboga mboga.

Na mimi niletewe steki ya nyama ya ng’ombe na viazi mviringo.

Na mara tu alipoondoka mhudumu Joji akamwambia Adam:

Haya bwana tuko katika furaha hoteli, furaha ambayo watu wengi hawaipati katika zama hizi kama unavyo sema wewe.

Hahahaha! naam, mashaka na wasiwasi yanauwa maana halisi ya maisha. Watu wamekuwa kama ala na ngao katika mashine isiyofanya kazi harakati zao hazina maana zimefungwa wala hazina athari. Na hawaoni raha na utamu wa maisha, wao wamekuwa kama mashine au vyombo vya kufanyia mambo hawajui furaha ya maisha ambayo ndani yake wanaishi wala hawajui mwelekeo wao ni wapi.

Hivyo wewe ni miongoni mwa wafuasi wenye kukimbia wasiwasi na shaka na kujisalimisha maishani kibubusa?

La! hapana siyo hivyo. Kukimbia kunamfanya mtu akaishi maisha magumu zaidi hata akijidhihirisha kinyume chake. Hebu angalia hapa mtu wa kwanza ana njaa kisha anasema ana njaa na wa pili ana njaa akipiga miayo lakini anasema anataka kulala!

Hahaha, wote wawili wana njaa!

Wa kwanza ana akili na mwerevu anajua mwili wake unahitaji nini na anaweza kuishi na nafsi yake.

Niambie kwa ukweli kabisa hivi wewe una furaha?

Hahahaha! unataka jawabu kwa wepesi huu? Naam. Furaha ni muono wa nafsi zetu na maisha yetu na ulimwengu na maumbile yake kwetu katika nafsi zetu.

Naogopa usije ukawa una furaha kama alivyo mke wangu ambaye ni mchaMungu kama wewe ulivyo ambayo (kwa maelezo yako) anayakimbia majibu kwa kukesha na kunywa!. Kisha akakaa kimya kidogo, akaendelea kwa kusema: nini maana ya maisha uonavyo wewe?

Mtu anaye kwepa maswali ya msingi hawezi kujihisi kuwa na furaha kamwe hata akiwa mtu wa dini kama asemavyo yeye. Ama swali juu ya maana ya maishajibu lake ni mrejesho wa upangaji wa maswali matatu: Kwa nini tumeumbwa? Kwa nini tunaishi? Ni wapi tunakoelekea?

Nini jawabu la maswali hayo?

Hivi wadhani kuwa yupo mtu anaye hisi na kuonja raha ya furaha anaishi kwa furaha lakini hajui majibu ya maswali haya!

Ni jibu kwa uwazi. Je unafahamu majibu ya maswali haya?

Mimi nadhani nina majibu ya wazi na yenye kukinaisha kwangu. Lakini siyo majibu ya kukuorodheshe wewe mawazo. Wewe unajua sana zaidi yangu juu ya mambo haya. Mimi ndio kwanza bado mwanafunzi katika Chuo Kikuu ninasoma mambo ya dini mbali mbali. Lakini wewe ni mhandisi mkubwa. Halafu majibu ya maswali hayo yanatokana na vile roho zetu na maisha yetu zinavyotoa majibu hayo. Hata kama ningelikuambia jibu, je lingekuwa na maana yoyote kama siyo sehemu ya roho yako na fikra zako?

Ah! wewe unanikumbusha kikongwe mmoja nilikutana naye njiani. Alikuwa anasema kuwa ana furaha na akaniambia hayo unayosema sasa.

Je, unakusudia kuwa mimi ni mwenye busara kama azungumzavyo mtu aliyepata uzoefu mkubwa wa maisha na akafahamu, au unadhani kuwa mimi ni mtu ninayecheza na falsafa ya maneno matupu yasiyo na maana. Kwa namna yoyote ile majibu ya maswali yanatokana na azima yako binafsi.

Hayo ndiyo maneno ya yule kikongwe! niazimie nini?

Azimia kupata majibu ya maswali haya kutoka katika nafsi yako ili uwe na furaha maishani mwako kisha akamkazia macho Joji: hebu nikuuliza swali: hivi unafikiri wapi tunaweza kupata majibu hayo?

Ah! sasa umehamia kule alikojikita dokta, hivi sasa hapo ulipo ni kama dokta!

Kicheko kikamtoka Adam, na akaendelea na maneno yake:

Hahahaha! wewe mbona unachanganya mambo hivi? Dokta gani huyo unayemsema? au yule kikongwe alikuwa ni dokta?.

Ah! samahani Ah! inaonekana kuwa nimechoka. Hapana huyo ni Kikongwe, Mimi naenda kutibiwa kwa dokta kwa lengo la kupata furaha. Haya maswali miye yamenichosha na hivi nimo katika hali ya kusumbuka na masikitiko.

Maswali hayo yamefikia kiasi cha kukutia masikitiko na kukosa raha kiasi cha kutafuta dokta? Nakuhakikishia kuwa hutopata jibu nje ya nafsi yako na maisha yako. Kwa ujumla nini maneno yanayofanana na ya dokta?

Alisema: Kabla ya kuanza kutafuta majibu lazima tujue hayo majibu yatatoka wapi?

Kwa mwangalio wangu hii mimi naona kuwa ni njia sahihi na nyepesi. Na jambo likifanywa kwa wepesi huwa ndio ufunguo wa ufumbuzi wake na mwanzo wa kuelekea kwenye uhakika wa mambo. Ama kuyafanya mambo magumu ni dalili ya kushindwa, tabu na kuchoka, inaonekana dokta wako ni mweledi wa mambo na ni mzuri. Je, ndivyo alivyo?

Kwa ueledi wa mambo na kutumia mantiki ni sawa, lakini kwa uzuri sidhani hivyo, ni mtu ambaye hafurahishi na inaonekana kuwa huyo bwana hana tabia nzuri.

Utafanya nini?

Sijui, nafikiria kuendelea naye hadi nipate matokeo yake, hata hivyo nijibu: hivi majibu tutayapata wapi?

Samahani, sitaki kupingana na daktari, daktari amekwambia nini?

Joji alicheka kwa jibu la Adam, pamoja na kuhisi kuwa anamsukuma kutoa majibu, joji alikuwa akifurahi kwa namna Adam anavyozungumza na kukwepa mtego wake hataki kutoa majibu, ndivyo inavyoonesha, lakini kwa nini hivyo?

Aliniambia: tafuta majibu mwenyewe, na akaniuliza kuhusu: majibu tutatoa wapi? Nini dhamana ya usahihi wa majibu yenyewe?

Mwanzo mzuri, unavutia na mwepesi na wa ndani kabisa, hata hivyo mimi siyo dokta wa kusema hayo ndiyo au kupinga hilo na kuweka sawa rai ya dokta.

Wapi tutapata majibu haya?

Tafuta katika roho yako pale unaposoma madhehebu na dini mbali mbali.

Katika madhehebu na dini mbali mbali!!

Naam katika madhehebu; na kama sio katika madhehebu na dini mbali mbali, je, wataka tutafute katika upagani?!

Kiasi gani nachukia upagani! Ni kuchanganyikiwa kwa akili na elimu.

Kama ni hivyo hatuna budi kutafuta katika madhehebu na dini mbali mbali.

Kuna uwezekano wa kusafiri kwenda India, penye fikra mbali mbali na dini mbali mbali, je, unadhani kwenda huko kutanisaidia kupata njia mbali mbali?

Mimi sio daktari kukuambia sawa au la, inafaa kumuuliza daktari, hata hivyo wacha nikuambie rai yangu kwa uwazi kabisa: Ni vizuri kufahamu njia mbali mbali za fikra na dini mbali mbali na madhehebu katika kupata majibu ya maswali haya, kadiri yatakavyokuwa mepesi ndivyo yanavyo karibia ukweli wa mambo.

Ni fanyeje ili kuweza kutumia madhehebu hizo na fikra tofauti hizo?

Naona uanze kwa kuangalia mambo kwa ujumla.

Vipi hivyo?

Tunaweza tukafuata njia mbili: Njia ya kwanza inayofuata mambo ya dini na nyingine ile ambayo inafuata upagani. Kama tulivyozungumza hapo kabla mimi ni moja ya njia hizo, njia inayofuata mambo ya dini, nadhani nilikuambia kuwa mimi ni mwanafunzi wa masomo ya Kidini?

Akaja mhudumu na vyakula walivyokuwa wameagiza, Joji akawa anataka wakomee hapo ili asimkere mgeni wake! Mgeni ambaye anakaa naye kwa mara ya kwanza, lakini alikuwa amemzoeya sana kama kwamba walikuwa wanafahamiana kwa muda mrefu.

Sasa sipendi nikusumbue katika kipindi hiki cha chakula. Kwa kweli mimi nahitajia unisaidie, pamoja na kuwa ni hivi karibu tu nimekufahamu ufahamu wa juu juu, lakini hisia yangu navutika sana na mazungumzo yako na nataraji kwa hilo sitokuwa nakusumbua.

Hahahaha! hunisumbui kabisa, inanitosha mwaliko wako wa chakula na haswa zaidi katika hoteli ya furaha! cha muhimu ule kwanza.

Walipokuwa wanakula, Joji alijaribu kubadilisha mwelekeo wa mazungumzo yao, akaona kuwa wakati umefika wa mazungumzo kuhusu chakula, huenda muelekeo wao wa mazungumzo kuhusu falsafa ukapungua kidogo..hata hivyo muda mrefu haukupita ila mazungumzo yao ya awali yakarudia..kwake Joji ana ufedhuli wa kujua na Adam mjanja wa kukwepa kutoa majibu.

Kwa nini njia ya dini ni bora kuliko ya upagani? Kwa mnasaba daktari wangu ni mpagani na anapinga dini zote na kuzidharau.

Pamoja na kufahamu kutoka kwako kuwa yule daktari ni hodari, ila naamini kuwa wapagani ndio watu wenye dhiki na wenye kukimbia nafsi zao. Ama kwa nini njia ya dini kuliko ile ya upagani? Hili lina vidokezi vingi tunaweza kuvifupisha katika nukta zifuatazo:

Kwanza: Je, inawezekana kufahamu kwa nini tuliumbwa kuliko anavyofahamu muumba wetu? Kwa njia nyingine ni kuwa si mimi wala wewe kutaka kuelewa kwa nini tuliumbwa ila kutoka kwa muumba mwenyewe. Njia ya upagani inakataa uwepo wa muumba na Mola wa walimwengu.

Pili: Upagani unajipinga wenyewe katika kila hali ya umbile lake. Unadhani kuwa ulimwengu unakwenda kulingana na vitu vidogo vidogo ambavyo havibadiliki –atom – ambavyo vilitokea ghafla bila mpangilio au muumba.

Tatu: Hao wapagani wanaficha imani kwa Mungu ndani ya nafsi zao, lakini linadhihiri mara wafikwapo na jambo au msiba, jambo la kwanza watakalosema ni–Ah Mungu wangu!

Nne: Nakwambia kwa uwazi kabisa hivi upagani ni jambo la ukweli au ni nia yakutaka kukwepa ukweli wa mambo? Hata wakikwepa mazigazi tatizo roho na nafsi zao bado zipo zinawasuta.

Hoja moja tu hapa inatosha kuvunja upagani! Na je, Kama zitakusanywa zote upagani hautasimama. Nadhani naafikiana nawe, hakuna haja ya kukamilisha. Upagani ni njozi tupu mtu akiufuata anajiona ana maarifa na elimu kubwa lakini ni kazi bure hamna kitu bali ni kupoteza muda na akili tu– huko ni kuweka misingi ya uongo tu – mtu anajiongopea yeye mwenyewe kabla hajaanza kuwaongopea watu. Naongezea hapo sasa tufuate dini gani? Maana dini ziko nyingi wingi wake kama idadi ya watu. Kisha akacheka na akasema: Pengine hizo dini ni nyingi kuliko watu wenyewe!

Naafikiana nawe kabisa, wanasema idadi ya dini zilizopo ni zaidi ya elfu kumi (10,000) na katika dini moja kama vile Ukristo kuna makundi 33,830, lakini si afadhali tuangalie kwa ujumla wake?

Ah una maana gani?

Tumeweka mafungu mawili ya mfumo na njia ya kuendea jambo hili moja la wale wenye kuamini kuwepo muumba na la pili la wapagani au siyo hivyo?

Bila shaka!

Basi kwa mwangalio wa jumla dini na imani ni mafungu mawili. Ama kuna dini ambazo ni mfumo ambayo asili yake ni kutoka mbinguni kwa Mwenyezi Mungu na kuna dini zingine ambazo zimechipuka hapa hapa ardhini ikiwa ni utunzi wa mwanadamu.

Nimeelewe nini unalenga. Sasa ni aina gani kati ya hiyo ni bora?

Achana na rai yangu, je hukuniambia kuwa utasafiri kwenda India.

Naam, sasa safari yangu ina uhusiano gani na mazungumzo yetu?

Bara Hindi lina utajiri mkubwa wa fikra na dini mbalimbali na madhehebu nyingi zinginezo kutoka ardhini na nyengine za mbinguni. Ukiwa India unaweza kupata fursa ya kulinganisha baina ya dini ya kutoka mbinguni na zile zilizozuliwa hapa ardhini. Utaziona ziko vipi kiuhalisia na siyo kusikia habari za kusifiwa tu ziko vipi.

Pamoja na kuwa msimamo wangu uko wazi juu ya hilo sioni tatizo kama kuakhirisha mjadala mpaka nitakapo rejea kutoka India. Lakini ninaswali moja: hivi unaamini kuwa kwa utaratibu huu nitaweza kufikia kwenye majibu ya maswali haya!

Uongofu na mafanikio ni fadhila zake Mwenyezi Mungu. Kama ukiwa mkweli katika utafiti wako nadhani utafikia kilele; la muhimu ni kuwa uwe na utashi na ukweli na weka mwelekeo wako katika hayo, na hakikisha kuwa unachukua mambo kwa wepesi na sio kwa uzito wake, na katika hali ya furaha na siyo katIka hali ya huzuni.

Umerejea katika maneno ya kikongwe.

Naweza kumwona wapi kikongwe huyu?. Hakika kanikonga roho yangu.

Sijui! Kwa hakika sijui. Nilikuwa katika hali mbaya, naye ndiye aliyechukua namba yangu ya simu na kusema atanipigia lakini mimi sikuchukua namba yake. Kwa mnasaba huu je waweza kunipa namba yako na anuani yako ya barua pepe?

Adamu aling’oa kipande cha karatasi kutoka kidaftari kidogo ambacho alikuwa nacho. Aliandika namba ya simu yake na anuani ya barua pepe na anuani ya face book yake na kumpa Joji:

Niwie radhi, mimi ni mhudumu tu wa mkahawa kama unavyoelewa –sina kadi yangu binafsi, ningekupa.

Ah! Hii inatosha kabisa, maana nataka kukuona mara nirudipo kutoka safari ya India je tumekubaliana?

Tumekubaliana.