Hekima ya Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) imepelekea kumtuma Muhammad (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) kwa ujumbe wake kwa watu wote wa ardhi, yenye kunasibiana na zama na mahala pote, Allah amesema: “Na hatukukutuma ila kwa watu wote, uwe mbashiri, na mwonyaji. Lakini watu wengi hawajui.” (34:28),
Na akauhifadhi (ujumbe huo) kutokana na kubadilishwa na kugeuzwa; ili ujumbe wake ubakie hai watu wanaishi nao, ikaepushwa na upotofu na kubadilishwa na kwa ajili hiyo Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) akaufanya kuwa ni ujumbe wa mwisho, na akamhusisha nao Muhammad, kwa sababu yeye ndie mtume wa mwisho, hakuna nabii baada yake; kwa kuwa Allah amekamilisha kwake ujumbe (utume), na akahitimisha kwake sheria na akatimiza jengo lake.
Kwa ajili hiyo Allah amekifanya kitabu alichokuja nacho Muhammad kuwa ni mtawala juu ya vitabu vilivyotangulia na kinachovifuta, kama vile ambavyo sheria aliyokuja nayo Muhammad (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) kufuta sheria zilizomo kwenye vitabu vilivyotangulia, Allah mwenyewe amedhamini kuhifadhi ujumbe wake; na hivyo ikawa inanukuliwa na kupokewa hali ya kuwa ni tawaatur; na hivyo ndivyo ilivyonukuliwa na kupokewa Qur-aan ikiwa ni tawaatur kwa sauti (jinsi isomavyo) na kwa kuandikwa jinsi iandikwavyo, kadhalika sheria ya dini hii na ibada zake zimenukuliwa jinsi ilivyokuwa ikitendwa kunukuliwa kwa njia ya tawaatur na sunnah zake na hukumu zake mbali mbali.
Mwenye kuangalia katika vitabu mbali mbali vilivyonukuliwa Sira na Sunnah za Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) ataona kuwa sahaba zake (Radhiya LLahu ‘anhum) waliweza kuwahifadhia watu hali za Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam), maneno yake yote, na matendo yake, na hivyo basi wakanukuu ibada zake kwa Mola wake na dhikri zake, istighfaar, jihadi zake, ukarimu wake, ushujaa wake, namna alivyokuwa akiishi na sahaba zake na wanaomtembelea, kama walivyonukuu furaha yake ilivyokuwa, huzuni yake, safari zake na kutosafiri kwake, wasifu wa kula na kunywa kwake, na kuvaa kwake, kuamka na kulala kwake,utakapojua hilo utayakinisha kuwa dini hii imehifadhiwa kwa Allah kuuhifadhi,na wakati huo utajua kuwa yeye ni hitimisho la mitume na manabii; Allah amesema: “Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Manabii, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.” (33:40).
Allah amemtuma Muhammad (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) kuwa rehma kwa walimwengu wote wanaume kwa wanawake, watoto kwa wakubwa, bali Allah amemtuma kuwa rehema hata kwa wasiomuamini, na rehema hii inaonekana wazi katika misimamo ya Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) maisha yake yote, na mingi inaonekana alipokuwa akilingania watu wake (akiwahurumia) walimkadhibisha na kumfukuza kutoka katika mji wake Makkah na kujaribu kumuua, Allah akawa ndiye anayemtosha kwa kila kitu akawarejeshea vitimbwi vyao Allah amesema: “Na walipo kupangia mpango walio kufuru wakufunge, au wakuuwe, au wakutoe. Wakapanga mipango yao, na Mwenyezi Mungu akapanga yake. Na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa mipango.” (8:30)
Na yote hayo hayakumzidishia isipokuwa rehema, huruma na kujali zaidi katika kuwaongoa, Allah Ta’ala amesema: “Hakika amekwisha kujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma.” (9:128),
Na baada ya kuwashinda katika siku ya ukombozi wa Makkah aliwasamehe, na Allah alipomtuma Malaika ili awabamize Makafiri kwa milima miwili mikubwa ili waangamie, Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) alisema: “Bali nitasubiri huenda Allah akatoa ndani ya migongo yao wenye kumuabudu Allah peke yake”
Allah Ta’ala amesema: “Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote.” (21:107),
Yeye ni rehema kwa Walimwengu, kwa watu wote pamoja na tofauti walizonazo za rangi zao, lugha zao, mitazamo yao, fikra zao, itikadi zao na sehemu zao.
Rehema hii haijaishia kwa wanadamu tu, bali imefika hadi kwenye wanyama na vitu visivyo na uhai. Kwa mfano yule ngamia wa mmoja wa wakazi wa Madina ambaye aliadhibiwa na mwenye ngamia akawa anamtesa kwa njaa kali, kwa hiyo moyo wa Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) ukamhurumia na kuamuru mwenye ngamia kumfanyia wema ngamia wake na kutomtumikisha zaidi ya uwezo wake.
Mara moja Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) alipoona mtu amechukua vitoto vya njiwa alimhurumia njiwa yule na kuamrisha kurejeshewa vitoto vyake, naye Mtume ndie aliyesema: “Na mnapochinja chinjeni vizuri.” (Muslim).
Kama ambavyo huruma ya Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) ilivyoenea kwa vitu visivyo na roho, alilihurumia lile gogo ambalo lilisikitika na kulia kwa kuachana na Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) hivyo akalihurumia na akateremka (kutoka mimbarini) na kukikumbatia hadi kiliponyamaza na kutulia.
Huruma yake haikuwa kwenye mitazamo na matukio peke yake, bali ni amri, sheria, mfumo na tabia njema ambayo ameifanya kwa ajili ya watu.
Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) amenukuliwa akisema katika kuhamasisha huruma, wema na ulaini kwa watu, na akaonya na kutahadharisha atakayefanya ugumu juu yao, akasema: “Ewe Mola wangu atakayetawalia jambo katika Ummah wangu akawafanyia watu ugumu, mfanyie ugumu, na atakayetawalia jambo katika umma wangu akawahurumia basi mhurumie.” (Muslim).
Hivyo basi rehema (huruma) ni tabia njema katika tabia njema za Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam), na msingi muhimu katika dini ya Kiislamu ni kuwa dini hii ni ya huruma na amani.
Utume wake Muhammad (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) umekuja kwa hiyo watu wakaongoka kwa baraka za utume wa Muhammad (Swala Llahu ‘alayhi wasallam), na ubainifu na uongofu, aliyokuja nayo (hidaya). Uongofu ambao uko wazi kuliko maelezo ya wanaousifia na kuwa juu ya maarifa ya wajuzi.
Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) alikuja na elimu yenye manufaa, matendo mema, tabia tukufu kabisa, mwenendo ulionyooka, ambao lau zingekusanyika hekima zote na elimu za watu wote na Ummah zote na matendo yake kulinganisha na hekima aliyotumwa nayo Muhammad (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) basi zingetofautiana na tofauti kubwa, kuhimidiwa ni kama apendavyo mola wetu na kuridhia.
Kwa upande wa akida; shirki ilikuwa imeenea kwa wanadamu na kumuabudu asiyekuwa Allah, kutokana na watu waliopewa kitabu kutoka mbinguni ambavyo vilipotoshwa.
Kwa hiyo Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) akaja na tawhidi halisi na kumuabudu Allah peke yake na kutomshirikisha na chochote, na kuwatoa watu katika kuabudu watu na kuelekea kumuabudu Mola wa waja, hivyo kutakasa nafsi zao kwa tawhidi na kuondosha uchafu wa ushirikina na uchafu wa kuabudu asiyekuwa Allah. Hivyo Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) akamtuma kwa yale aliyowatuma nayo Mitume kabla yake, Allah amesema: “Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimfunulia ya kwamba hapana mungu isipo kuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu.” (21:25),
Na akasema Allah vilevile: “Na Mungu wenu ni Mungu mmoja tu, hapana mungu ila Yeye. Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.” (2:163).
Kwa upande wa kijamii, Muhammad (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) alitumwa zama ambazo dhuluma, udikteta na kuabudiwa watu kulikuwa kumetawala, utabaka unaochukiza ulikuwa umewagawa wanadamu katika tabaka nyingi, kila tabaka linatumikisha tabaka lingine na yanadhulumiana, Mtume Muhammad (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) akaja na kuwafanya watu wote kuwa sawa, Muarabu kwa Muajemi, mweupe kwa mweusi, hakuna mbora ila kwa ucha-Mungu na amali njema, Allah amesema: “…Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi...” (49:13)
Na akaamrisha uadilifu, wema, kushikamana kijamii na kukataza dhulma, munkari na uadui, Allah amesema: “Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu, na hisani, na kuwapa jamaa; na anakataza uchafu, na uovu, na dhulma. Anakuwaidhini ili mpate kukumbuka.” (16:90)
Bali akahifadhi haki za watu, na kukataza kundi moja kudharau kundi lingine, Allah amesema: “Enyi mlio amini! Wanaume wasiwadharau wanaume wenzao, wala wanawake wasiwadharau wanawake wenzao. Huenda hao wakawa bora kuliko wao. Wala msivunjiane hishima, wala msiitane kwa majina ya kejeli. Ni uovu kutumia jina baya baada ya kwisha amini. Na wasio tubu, hao ndio wenye kudhulumu.” (49:11).
Upande wa tabia; Allah amemtuma Mtume wake na tabia za watu zilikuwa duni, chafu na mbaya sana, hakukuwa na maadili mema wala tabia njema, Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) akaja kuwarudisha watu kwenye maadili mema na adabu tukufu; ili maisha yao yafurahi kwa miamala mizuri, Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) amesema: “Kwa hakika nimetumwa kutimiza mazuri ya tabia.” (Al-Bayhaqi).
Bali Allah amesifu tabia yake kuwa ni tukufu; Allah amesema: “Na hakika wewe una tabia tukufu.” (68:4),
Nae alikuwa ndie kiigizo chema katika tabia na adabu, na mfano mzuri katika kuipa nyongo dunia, Ucha-Mungu na muamala – mzuri na maneno mazuri bali Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) alikuwa ni kigezo kizuri katika kila kitu kizuri, Allah Ta’ala amesema: “Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anaye mtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana.” (33:21).
Ama mwanamke alikuwa anasumbuka kwa mengi kabla ya Allah kumtuma mtume wake, wakati huo mwanamke akidhalilishwa na hana haki yoyote, watu walitofautiana kuhusu mwanamke; Je, ni mwanadamu au la? Je, ana haki ya kuishi au huuawa na kuzikwa akiwa mdogo?! Watu walikuwa kama vile walivyosifiwa na Allah (Subhaanahu wa Ta’ala): “Na mmoja wao akibashiriwa kwa msichana, uso wake unasawijika, naye kajaa chuki. Anajificha asionekane na watu kwa ubaya wa aliyo bashiriwa! Je, akae naye juu ya fedheha hiyo au amfukie udongoni? Tazama uovu wa wanavyo hukumu!” (16:58-59),
Alikuwa ni mdoli tu anachezewa na watu na kustarehesha, akiuzwa na kununuliwa, kiumbe kinachodharauliwa, hivyo Allah hivyo Allah akamtuma Mtume wake kwa ajili ya kumtukuza, kumkirimu mwanamke, Allah Ta’ala amesema: “Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri.” (30:21),
Bali aliamrisha afanyiwe wema kama mama, Allah amesema: “Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema….” (17:23),
Na wema kwake ukatangulizwa kuliko wema wa mwanaume, wakati mmoja mtu alikwenda kwa Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) na kusema: “Ewe Mtume wa Allah, ni nani mwenye haki zaidi ya kusuhubiana nae? (Mtume) akajibu: “Ni Mama yako”, akasema: kisha nani? Akasema: “Mama yako”.
Akasema: “kisha nani?” Akasema: “Mama yako”. Akasema kisha nani? Akasema: “Baba yako.” (Al-Bukhari).
Kadhalika Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) ametaka akirimiwe akiwa ni msichana, akasema (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam): “Aliye na wasichana watatu anawalea, kisha akawahurumia, na kuwatunza, mtu huyu imempasa pepo kabisa amesema: ilisemwa: Ewe Mtume wa Allah, Je, akiwa na wawili (Mtume) akasema: “Na wawili:” (Imepokewa na Ahmad).
Vile vile mwanamke huyo akiwa ni mke ameamrishwa apewe hadhi yake kwa kuunganishwa na wema wake, hivyo Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) akasema: “Mbora wenu ni Mbora wenu kwa familia yake, na mimi ni Mbora wenu kwa familia yangu.” (Imepokewa na Ibn Majah).