Utafutaji wa hotel inayofaa ulimaliza siku yote iliyobakia baada ya marafiki wawili walipowasili Paris, mwishowe walifikia katika Hosteli ya Vijana wa Paris, dhahiri ilionekana kuwa wana haja ya mapumziko; walimalizia usiku uliobakia usingizini, siku iliyofuatia marafiki wale wawili, walitoka ili kuufahamu mji na alama zake, katikati ya kuzunguka kwao walipita katika mgahawa mmoja….
Maiko: Unaonaje Rashidi tuingie tupate kikombe cha chai na tupumzike kidogo kwenye mgahawa huu.
Rashidi: Hamna kizuizi, kweli nami ninahisi nahitaji kupumzika kidogo.
Maiko: Katika mgahawa huu alikuwa akikaa Sigmund Freud, yule tabibu nafsi mashuhuri, je, ulishawahi kumsikia?
Rashidi: Ndio, yule ambaye jina lake linahusishwa na skuli ya uchambuzi wa nafsi katika saikolojia, na kadhalika anahusishwa vile vile katika kulingania katika uhuru wa vidhibiti vya kimaadili na kuhalalisha mambo ya kijinsia.
Maiko: Kwetu sisi ni mwanazuoni mwenye hadhi yake bila ya kujali hayo uliyoyataja.
Rashidi: Ninadhani ni moja katika nguzo za fikra ambayo imeumba ustaarabu mpya katika jamii za nchi za Magharibi, akiwa pamoja na Darwin, Immanuel Kant, Karl Marx, Émile Durkheim na Sater, kila mmoja katika wao amesimama kwa nafasi yake katika kutingisha fikra za watu wa Magharibi na kurejesha mfumo wake katika hali inayotakiwa kulingana na matakatifu mapya ya Magharibi….na kila mmoja katika wao alifanya kazi ya kubomoa: dini, maadili na desturi za watu.
- Nadharia ya Darwin ya ukuzi na maendeleo ilikuwa ni cheche ambayo ilituma makombora mawili ya hatari ya kifikra, walioitumia waliokuja baada yao ili kupiga miundo mbinu ya kifikra wakati huo; Kombora la kwanza: Kueneza fikra ya ukuzi yenye kudumu ambayo inapuuza fikra ya kuthibiti (yaani mwanadamu habadiliki) baada ya hapo ni ukiasi wa kila msingi wa mambo ya maadili, fikra na taswira mbali mbali..
Kombora la Pili: Fikra ya uhayawani wa mwanadamu na umaada wake na umaada wa vipengele vyenye kuathiri ndani yake, pamoja na kupuuzia kukubwa nafasi ya roho, na kupinga kuwa mwanadamu kaumbwa na Mungu, kwa hiyo ukawa mwanzo wenye nguvu wa kubomoa ufahamu muhimu kuhusu maswali makubwa ya kifalsafa kuhusu Mungu, mwanadamu, ulimwengu na marejeo ya mwanadamu.
Ama nafasi ya Freud ilikuwa ni kumuweka mwanadamu katika fundo za kijinsia, na akapinga kuwa mwanadamu anaelekezwa na akili katika maadili yake, na akasema kuwa kitu cha msingi chenye kumsukuma mwanadamu katika maisha yake ya kila siku ni ladha, na kutokea hapo mifumo yote ya kimaadili imevunjika na kubomoka na hiyo kuonekana kuwa ni kukosa maendeleo na kurudi nyuma, na mtu wa namna hii kuonekana ni mtu asiyeishi katika hali halisi na kukosa kuwa mtendaji.
Maiko: Naamini kuwa kuna dondoo zenye kushirikiana baina ya ustaarabu wa wanadamu, kadhalika pia kuna dondoo ambazo kila ustaarabu unatofautiana na mwingine, kwa mfano mitazamo hii, ‘Mungu, mwanadamu na ulimwengu’ ni vitu ambavyo jamii zote hushirikiana, hata hivyo kila ustaarabu hutofautiana na mwingine katika mitazamo hii; moja katika staarabu hizi zimeshinda mtazamo mmoja kuliko mitazamo miwili iliyobakia na hivyo huonekana katika mtazamo wa kwanza.
Katika ustaarabu wa Ulaya leo hii, na baada ya zama za mwamko, mtazamo kuhusu ulimwengu ulitawala katika ustaarabu huu, na pindi fikra za kisomi na kisayansi zilipoenea katika jamii ya Kimagharibi zama zile, zilifuta fikra ya kuwa mwanadamu kaumbwa na Mungu na kuja kwa mtazamo wa kimaada, na hivyo basi kuua kabisa mtazamo wa kiroho kwa mwanadamu, kwa hakika Darwin alikuwa katika wanafikra wakubwa aliyeasisi muelekeo ule.
Rashidi: Nakubaliana nawe kabisa katika hilo, lakini nitakubainishia baadhi ya uliyosema:
Kwanza: Sababu ya msingi na kubadilika kwa fikra hizi hadi kuwa mapinduzi ya kweli kwa wakati ule ni uwepo wa hali fulani ya faragha ya kiroho na kielimu katika jamii ya kimagharibi wakati ule, ongeza na utawala wa Kanisa na kung’ang’ania kwake rai zake mbovu kuhusu maumbile na uhai pamoja na itikadi yake ya kuwalazimisha watu kuamini rai zile.
Pili: Ni kuwa katika makosa yaliyoenea ni kuitakidi kwamba sababu ya maendeleo ya nchi za Magharibi ni kutegemea kwao rai na nadharia ambazo zilienea mwanzoni mwa mwamko ule na katikati yake.
Tatu: kuwa rai na nadharia za wanafikra na wanafalsafa hao zilianza kupungua na kuondoka moja baada ya nyingine baada ya mapinduzi ya kweli ya kisayansi, pamoja na hayo ni kuwa wenye uwezo mdogo wa utamaduni huko Magharibi na Mashariki bado wameangukia katika kuathirika na propaganda ambazo zinategemea rai zile.
Ama mazungumzo yako kuhusu kushirikiana kwa ufahamu baina ya mitazamo ya staarabu ni kuwa umenikumbusha ulinganisho (mzuri) wenye kuvutia kati ya nadharia ya Freud katika kufasiri mfumo wa mwanadamu na maneno ya mwanazuoni mmoja wa Kiislamu, yameandikwa inakaribia miaka mia saba.
Maiko: Nzuri sana kuwepo mfanano kati ya maneno ya Freud na mtazamo wa mwanazuoni wa Kiislamu zama zile.
Rashidi: Sio kufanana kwa mtazamo, bali kufanana kwa kile tunachoweza kukiita mfanano wa umbo, ili nikubainishie zaidi: Je, unafahamu mjengo wa mfumo wa nafsi kulingana na Freud?
Maiko: Ndio, naufahamu vizuri sana, kwa ufupi ni kuwa Freud alifikiria kuwa madamu mwanadamu ana mifumo mingine ya kibaiolojia inayoratibu uhai wa mwanadamu kama vile mfumo wa chakula au mfumo wa damu na mingineyo, hivyo basi mwanadamu nae ana mfumo wa nafsi ambao una sehemu zenye uhusiano baina yake.
Na mfumo huu una kile alichokiita: (Id), (Super Ego) na (Ego).
(Id), Ni sehemu inayohusika na silika na matamanio binafsi yenye kumsukuma mtu pamoja na uzoefu uliojificha na mielekeo ya awali ya kijima yenye msukumo wenye kuendelea katika sura ya upofu ili kujitokeza katika sehemu ya hisia, kwa lengo la kutekeleza na kufanikisha matamanio kulingana na msingi wa ladha, (Id) ni mfumo wa kale zaidi wa nafsi uliojengeka, (Id) ina yote ayabebayo mwanadamu pindi anapozaliwa na kila ambacho kitakachoainisha umbo lake maalum, hivyo basi (Id) inawakilisha alichokirithi mtu.
Ama (Super Ego) tunaweza kuuelezea kuwa ni mlolongo wa maadili ya jamii husika na misingi ya maadili mema, yaani: Yale ayapatayo mwanadamu kutoka kwa wengine; na inakusanya athari za malezi na tabia azipatazo mtoto kutoka kwa wazazi wake, shule na jamii, athari za desturi ya familia yake, kabila au ukoo wake, taifa na dini, pamoja na muktadha wa jamii inayomzunguka moja kwa moja, pia (Super Ego) inaathirika pindi mtoto anapokuwa na walezi wanaowawakilisha wazazi wao au mbadala wao, kama vile baadhi ya walezi na watu ambao wanawakilisha ruwaza njema za jamii…katika (Super Ego) inamili kuwa mbali kabisa na matendo yote ya matamanio na ya kisilika, ambapo hiyo (Super Ego) ni sehemu ya dhamira ya mtu, nayo ni sehemu au eneo linalohusika na maadili mema yaliyo mbali na uhalisia, matilaba yake siku zote ni kufikia ukamilifu na sio katika ladha kulingana na Freud.
Ama Ego unaweza kuuelezea kuwa ni matokeo ya mgongano au maafikiano kati ya (Id) na (Super Ego), kati ya matamanio yenye kusimama kwa msingi wa ladha na maadili yaliyosimama chini ya udhibiti na mipaka, hivyo basi (Ego) ni hisia zilizoamka ambazo zinafanya kazi ya kusuluhisha matatizo yenye kuibuka pamoja na hali halisi au kati ya matamanio baina yake ili kuhifadhi na kuweka sawa haiba ya mtu, nayo mwishowe ni matokeo ya haiba ya mtu inayoonekana katika tabia yake ya nje.
Kwa hiyo (Super Ego) ni ile sehemu iliyojitenga na (Ego) na kuidhibiti, na kwa ajili hiyo inasimama kama tahadhari kwa (Ego) kuwa chini ya utawala wa (Id) na kutekeleza matilaba ya matamanio yaliyojificha.
Rashidi: Ufafanuzi mzuri Maiko, unaelezea utafikiri Freud mwenyewe anazungumza kwenye mgahawa akiwa anakunywa kikombe cha chai.
Lakini nakamilisha maelezo haya mazuri, kuwa Freud anathibitisha ugumu wa kazi ambayo unaisimamia (Ego) katika mfumo wa Nafsi, na kazi hii ni ngumu (au haiwezekani kabisa) ni kusuluhisha matilaba kinzani, nayo ni juu ya (Ego) kuitika matilaba ya (Id) na ambayo kimsingi ni matamanio ya kijinsia, na wakati huo huo kuchunga matakwa ya nje yanayoizunguka (Super Ego) nayo ni mahitajio ya kimaadili na ya kijamii; na hivyo basi inaelekea suala la muwafaka baina yake kuwa ni gumu, na ndio maana (Ego) inajaribu kutengeneza mahusiano ya kufahamiana na muwafaka pamoja na (Id) na hujaribu kujibu na kushibisha hamu zake, na hivyo kugongana na (Super Ego) ambayo ni hali halisi ambayo inaratibu mahusiano ya kijinsia kulingana na vigezo husika ambavyo vinapelekea mara nyingi katika kuzuia matamanio ya kijinsia. Ikiwa (Ego) itaweza kuwafikisha mizani ya sawa kati ya (Id) na (Super Ego) pamoja na hali halisi, mtu ataishi maisha yenye muwafaka, ama ikiwa (Id) ikishinda au (Super Ego) ikitawala kwa mtu itapelekea hilo katika migongano; kushindwa kwa (Ego) kusuluhisha kati ya mahitaji na matakwa haya pinzani, hupelekea katika hali za maradhi.
Jambo lililo la hatari hapa: Tutakapo sema: Kuwa uzima wa Nafsi kwa mtazamo huu yaani (Ego) pamoja na (Id) kupata muwafaka; yaani: matamanio na matilaba ya kihayawani pamoja na (Super Ego); yaani misingi ya maadili mema, na kuwa kushindwa kutoitikia matakwa haya ya (Id) hupelekea katika kuficha hisia na matamanio, na kwa kuzingatia kuwa kutoweza kwetu kuibadilisha (Id)….haitobaki mbele yetu kufikia muwafaka huu isipokuwa kubadilisha (Super Ego) na kuiangamiza ikilazimika jambo hilo, hivyo basi ikawa hapana budi kuiondoa dini pamoja na maadili katika maisha yetu, na kuzibadilisha kwa maslahi yenye kukubaliana na matamanio ya mwanadamu na mahitajio yake ya kijinsia na ya kibinafsi ambayo yanatekelezwa na (Id). -Hili ndilo haswa lililotokea katika nchi za Magharibi pindi walipoondosha na kung’oa dini na maadili mema, na hivyo wakayapa uhuru matamanio na mahusiano ya kijinsia yasiyokuwa na udhibiti katika vifungo vya maadili na tabia njema, na ustaarabu wake kusimama katika hilo, familia ziliparaganyika baada ya hapo, bali utu wa mwanadamu ulipotea; ilipokuwa sasa huwezi kutofautisha kati yake na jamii ya Kihayawani isiyokuwa na akili ambayo haijui vidhibiti vya kimaadili nje ya maumbile yake na silika….naona kuwa sisi tunarudi tena kwa Darwin baada ya kuwa tumeanza nae.
Maiko: Unakusudia kusema: Ikiwa matamanio yaliyojificha na kuzikwa yatatafuta njia ya kushibisha (iwe ni moja kwa moja au isiwe moja kwa moja) hilo litapelekea kulingana na ufahamu wako kwa Freud na madhehebu yake kuwa ustaarabu ambao unasimamia maadili mema ni ustaarabu unaosimama katika kufukia hisia na kuzuia matamanio ya mtu.
Rashidi: Ndio, ustaarabu wa kimagharibi pindi unapotoa maadili mema hufanya hivyo kwa kuondosha utukufu wa Mwenyezi Mungu katika hesabu zao, wakati ambapo Waislamu wanaona kuwa maadili mema katika jamii za mwanadamu ni jambo la msingi kabisa na kuwa chanzo chake kiwe ni cha kisheria kutoka mbinguni na sio kwenye akili za wanadamu, kwa sababu akili pekee yake mwishoni itapotea, ama akili hiyo hiyo ikiwa ipo katika mipaka ya kisheria basi maadili yatakayopatikana kutokea hapo yatakuwa ni maadili mema.
Lakini hukuniambia mimi ewe Rashidi alichokisema mwanazuoni huyu kuhusu dini yenu ambayo umeizungumzia. Je, alichokisema kinawafikiana na maneno haya au vinapingana?
Rashidi: Kwa hakika alichokisema kipo katika mfumo unaotokana na maadili na mitazamo, na kukionesha katika mfumo huu na kuweka maneno yake katika mtiririko wake yatakuwa marefu, ninaona kuwa tuakhirishe hadi kikao kijacho.