Mwanadamu huyu ambaye Allah amemdhalilishia kila kitu katika Ulimwengu huu na kumkirimu yeye peke yake na kuwaacha viumbe wengine, Allah amemuumba kwa hekima kubwa sana; Allah ameepukana na mchezo na ubatili, Allah amesema: “Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kukhitalifiana usiku na mchana ziko Ishara kwa wenye akili, Ambao humkumbuka Mwenyezi Mungu wakiwa wima na wakikaa kitako na wakilala, na hufikiri kuumbwa mbingu na ardhi, wakisema: Mola wetu Mlezi! Hukuviumba hivi bure. Subhanaka, Umetakasika! Basi tukinge na adhabu ya Moto.” (190-191)
Kadhalika Allah amezungumzia kuhusu dhana potofu ya makafiri: “Na hatukuziumba mbingu na ardhi na viliomo ndani yao bure. Hiyo ni dhana ya walio kufuru. Ole wao walio kufuru kwa Moto utao wapata.” (38:27)
Allah hakumuumba mwanadamu kwa ajili ya kula, kunywa na kuzaa tu, na kwa mfano huo wawe sawa na wanyama, bali Allah Ta’ala amemkirimu na kumfadhilisha mwanadamu kuliko wengi aliowaumba lakini watu wengi wamekataa na wamekufuru; hivyo wakajifanya hawajui au kukataa hekima ya kweli ya kuumbwa kwao, hamu yao kubwa ikawa ni kustarehe kwa matamanio ya kidunia, na maisha ya watu hawa ni kama vile maisha ya wanyama, bali duni zaidi kuliko wanyama, Allah Ta’ala amesema: “…Na walio kufuru hujifurahisha na hula kama walavyo wanyama, na Moto ndio makaazi yao.” (47:12)
Katika aya zingine Allah amesema: “Waache wale, na wastarehe, na iwazuge tamaa. Watakuja jua.” (15:3)
Na: “Na tumeiumbia Jahannamu majini wengi na watu. Wana nyoyo, lakini hawafahamu kwazo. Na wana macho, lakini hawaoni kwayo. Na wana masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama nyama howa, bali wao ni wapotofu zaidi. Hao ndio walio ghafilika.” (7:179).
Watu wote wanalazimika kuamini kuwa viungo vyao vimeumbwa kwa hekima, huu ni uoni wa mazingatio kwa mfano masikio kwa ajili ya kusikilizia, na kadhalika…Je, inawezekana sasa viungo vya mwanadamu vikaumbwa kwa hekima halafu mwanadamu mwenyewe akaumbwa bila maana? Au ni kuwa haridhiki kumuitikia Mola wake ambaye amemuumba alipomjulisha hekima ya kuumbwa kwake?!
Hivyo basi ni kwa nini Allah ametuumba? Na kwa nini alitukirimu na kutudhalilishia kila kitu? Ametujulisha hilo Subhaanahu; Allah amesema: “Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi. ” (51:56),
Na Allah Mtukufu akasema vile vile: “AMETUKUKA ambaye mkononi mwake umo Ufalme wote; na Yeye ni Mwenye uweza juu ya kila kitu. Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Na Yeye ni Mwenye nguvu na Mwenye msamaha.” (67: 1-2),
Na kinachofahamika kwa watu wenye akili ni kuwa mwenye kutengeneza kitu ndiye mwenye uwezo wa kukielezea hekima yake kuliko mtu mwingine, na kwa Mwenyezi Mungu kuna mifano mikubwa, kwani yeye ndiye aliyemuumba mwanadamu, naye anajua zaidi hekima ya kuumbwa kwake. Ibada hapa ufahamu wake ni mpana mno, mkubwa kuliko Swala, Funga, bali inaingia ndani yake kuimarisha ardhi yote, Allah Ta’ala anasema: “…Yeye ndiye aliye kuumbeni katika ardhi, na akakuwekeni humo. Basi mwombeni msamaha, kisha mtubu kwake. Hakika Mola wangu Mlezi yupo karibu, anaitikia maombi.” (12:61)
Na maisha yote ya mwanadamu ni ibada kwake Allah amesema: Sema: Hakika Sala yangu, na ibada zangu, na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote. Hana mshirika wake. Na hayo ndiyo niliyo amrishwa, na mimi ni wa kwanza wa Waislamu.” (6:162-163).
Ikiwa Ulimwengu huu wote umedhalilishwa kwa ajili yako na dalili mbali mbali, alama zake na ushahidi mbele ya macho yako zenye kushuhudia kuwa: Hapana Mola apasaye kuabudiwa ila Allah Peke Yake hana mshirika, na pindi ujuapo Ewe mwanadamu ya kuwa ufufuo kwako na maisha yako na kufufuliwa baada ya kufa kwako ni jepesi mno kuliko kuumbwa kwa mbingu na ardhi, na ya kuwa Allah Ta’ala amekuumba kwa umbo lililo bora, na akakukirimu kwa takrima kubwa, na akakudhalishia Ulimwengu wote kwa ajili yako, sasa ni nini kikudanganyacho na Mola wako Mtukufu (hata ukamuasi)?! Allah amesema: “Ewe Mwanaadamu! Ni nini kikudanganacho na Mola wako Mtukufu Aliyekuumba.” (82:6-8)
Mwishowe wewe ni mwenye kukutana na Mola wako, Allah amesema: “Ewe mtu! Hakika wewe unajikusuru kwa juhudi kumwendea Mola wako Mlezi, basi utamkuta. Ama atakaye pewa daftari lake kwa mkono wa kulia, Basi huyo atahisabiwa hisabu nyepesi, Na arudi kwa ahali zake na furaha. Na ama atakaye pewa daftari lake kwa nyuma ya mgongo wake, Basi huyo ataomba kuteketea. Na ataingia Motoni. ” (84:6-12)
Nenda katika njia ya furaha ya duniani na Akhera kwa maisha kwa lengo na hekima ya kuumbwa kwako, na hapo ndipo utakapopata furaha kwa ajili ya maisha yako, na utapata utulivu na kufurahia kukutana na Mola wako baada ya kifo chako.
Ulimwengu wote upo katika kumuabudu Mola wake, viumbe wake wote wanamsabihi na kumhimidi Mola wao, Allah Ta’ala amesema: “…Viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi vinamtakasa Mwenyezi Mungu…” (62:1)
Na vinasujudu kwa ukubwa wake: “Je! Huoni kwamba vinamsujudia Mwenyezi Mungu viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi, na jua, na mwezi, na nyota, na milima, na miti, na wanyama, na wengi miongoni mwa watu. Na wengi imewastahiki adhabu. Na anaye fedheheshwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumhishimu. Hakika Mwenyezi Mungu hutenda apendayo.” (22:18).
Bali viumbe vyote hivi vinaswali kwa ajili ya Mola wake kwa swala inayonasibiana nao, Allah amesema: “Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu vinamtakasa vilivyomo katika mbingu na ardhi, na ndege wakikunjua mbawa zao? Kila mmoja amekwisha jua Sala yake na namna ya kumtakasa kwake…” (24:41),
Je, inakulaiki wewe kukosa kuhudhuria katika tukio hili lenye kutisha? Baada ya hapo utakuwa ni mwenye kufedheheshwa; amesema kweli Allah Ta’ala: “Je! Huoni kwamba vinamsujudia Mwenyezi Mungu viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi, na jua, na mwezi, na nyota, na milima, na miti, na wanyama, na wengi miongoni mwa watu. Na wengi imewastahiki adhabu. Na anaye fedheheshwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumhishimu. Hakika Mwenyezi Mungu hutenda apendayo.” (22:18)