Sharia ya Kiislamu inasifika kwa kuwa na haiba na utukufu wa kujali utu wa mwanadamu, na hivyo inatokana na sifa ya kidini iliyoshikamana nayo na kwa sababu muwekaji wake ni Allah ambaye yeye nafsi za wanadamu zinanyenyekea kwake na kutukuzwa.
Sharia ya Kiislamu ni kwa ajili ya Ummah na mataifa yote kwa tofauti zao zilivyo, tabia, mazingira na lugha-wanayozungumza; kwa sababu muwekaji wake (sharia hii) ni Allah (Subhaanahu Wa Ta’ala), naye ni mjuzi wa yaliyopo na yajayo kwa maumbile yao na silika ya tabia zao na kila chenye kuhusiana nao pamoja na kutakasika kwake kutawaliwa na matamanio, Allah amesema: “Basi uelekeze uso wako sawasawa kwenye Dini - ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilo waumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo Dini iliyo nyooka sawa. Lakini watu wengi hawajui.” (30:30),
Ama sharia hizi za wanadamu zimewekwa na mwanadamu nao pamoja na elimu kubwa waliyofikia elimu yao hiyo ina upungufu na hata wakijua ya jana yao na mambo yao ya leo, hawawezi kujua ya kesho yalivyo, na hata wakijua tabia za baadhi ya watu hawawezi kujua yote, katika hali hii. Sheria za wanadamu hazilingani na maumbile yote ya mwanadamu wala hazilingani na mazingira yote, na ikiwa sheria hiyo imefaa kutumika kwa watu fulani haifai kutumika kwa wengine….
Sharia ya Kiislamu inaafikiana na usawa, haki na uadilifu na hiyo ni kutokana na kutowezekana kutokea makosa, au dhuluma au kutawaliwa na matamanio na hamasa za watu, Allah Mtukuka amesema: “Na yametimia maneno ya Mola Mlezi wako kwa kweli na uadilifu. Hapana awezaye kuyabadilisha maneno yake. Na Yeye ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua.” (6:115),
Allah pekee ametakasika kuepukana na malengo (matamanio), mwenye kujua mambo yaliyofichikana na yaliyodhihiri, yeye ndie amezunguka mambo ya waja, hawezi kuamrisha ila lenye maslahi yao, wala hakatazi ila lenye kuwadhuru. Ama kanuni na sheria waliyojitungia wanadamu hukumbwa na makosa, usahaulifu, na kufuata matamanio ya watu, hivyo ni vigumu kusalimika na makosa, upungufu na mabadiliko, Allah Mtukuka amesema: “…Na lau kuwa imetoka kwa asiye kuwa Mwenyezi Mungu bila ya shaka wangeli kuta ndani yake khitilafu nyingi.” (4:82).
Sharia ya Kiislamu sio kanuni tu zilizowekwa na fikra za watu, lakini muwekaji wake ni Allah Aliyetukuka katika yale yaliyo mnasaba na mwanadamu na tabia yake na maumbile yake, Aliyeumba watu anafahamu zaidi yenye kunasibiana nao, “Asijue aliye umba, naye ndiye Mjua siri, Mwenye khabari?” (67:14),
Naye anajua zaidi anachomrahisishia: “Mwenyezi Mungu anataka kukupunguzieni taabu, na mwanaadamu ameumbwa dhaifu.” (4:28).
Ama sheria za wanadamu zimewekwa kulingana na matakwa ya aliyeiweka, na kulingana na umuhimu na mazingira yake.
Sharia ya Kiislamu inahusiana na matendo ya dhahiri na matendo ya ndani ya mwanadamu; Allah Mtukuka amesema: “…Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu anajua yaliyomo katika nafsi zenu. Basi tahadharini naye….” (2:235).
Kinyume na sheria za mwanadamu ambazo zinajihusisha na matendo ya nje ya mwanadamu tu na hayajali upande wa kiroho hata kidogo, ama adhabu zinazotolewa na sharia hizi za mwanadamu ni za kidunia tu.